Saturday, April 21, 2012

KWA NINI VIJANA WENGI HAWAJAKA KWENYE NAFASI ZAO KI-MUNGU?




KWA NINI VIJANA WENGI HAWAJAKA KWENYE NAFASI ZAO KI-MUNGU?

Na : Patrick Sanga.

Iyohana 2:14

 Kila kundi katika kanisa, jamii na hata nchi Mungu amelipa nafasi na wajibu wake maalumu wa kutekeleza. Pia Mungu anao mtazamo wake binafsi na matarajio yake kwa hayo  makundi
mbali mbali ndani ya nchi. Vijana, watoto, wababa, wazee, wanawake, viongozi wote / yote yana mtazamo wake mbele za Mungu. Ukimuuliza Mungu  nini mtazamo  wako  kwa vijana, atakujibu  soma vizuri IYohana 2:14 maana  yake Mungu anawatazama vijana kama watu wenye nguvu, watu ambao neno la Mungu linakaa ndani yao na pia wamemshinda mwovu.
 Sasa  ukirudi  mazingira  halisi unaona kwa  asilimia kubwa vijana wengi hawako kwenye nafasi ambazo Mungu aliwakusudia. Lengo la somo hili ni :--         Kueleza sababu za kwa nini  vijana wengi hawajakaa  katika nafasi zao.-         Kumweleza kijana mambo ya kujiepusha nayo ili  aweze kukaa kwenye nafasi yake.-         Kumpa kijana maarifa yatakayomsaidia kurejea kwenye nafasi yake na ili aweze kutekeleza matarajio ya Mungu kwake. Zaidi ujumbe huu umekusudia kulenga na kuelewesha vijana waliokoka, nazungumza  na vijana waliookoka maana hawa ndio ambao Mungu amewatamkia maneno haya au kuwa namtazamo huu juu yao. Zipo sababu  nyingi lakini hizi zifuatazo ni za msingi na zimesababisha wengi kuishi maisha nje ya kusudi la Mungu na kufa bila kutekeleza matarajio ya Mungu  kwao sababu hizo ni:-
-         Moja vijana wengi hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu.
 Biblia inasema katika matendo ya Mitume 1:8 kwamba “lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajia  juu yenu Roho  Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika  Yerusalemu, na katika uyahudi wote, na samaria, na hata mwisho wa nchi”. Hivyo vijana wengi hawajakaa katika nafasi zao  kwasababu wengi wa vijana leo makanisani  hawajajazwa nguvu za Roho Mtakatifu si kwamba  Mungu hataki kuwajaza lakini shida ipo kwa vijana wenyewe wengine kutotaka kujazwa nguvu hizo, lakini wengine hawajui nini wafanye wajazwe  nguvu za Roho  Mtakatifu  na wengine wanajua lakini hawana kiu ya kujazwa nguvu hizo.
         Pili vijana wengi hawajui namna ya kuenenda kwa Roho .
Paulo kwa warumi anasema” kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” Warumi 8:14 na pia kwa wagatia  anasema” Basi nasema  enendeni kwa Roho hamtatimiza kamwe   tamaa za mwili “Gal 5:16.         Kuna  wengi waliojazwa lakini si wote wanaoenenda au wanaoishi wa Roho. Vijana wengi Mungu amewapa  vitu vizuri  sana ndani yao lakini kwa sababu ya kukosa utiifu na kutoenenda kwa  Roho wameshindwa kusimama kwenye nafasi zao.    
Tatu  vijana wengi wameshindwa kushirikiana  na upako wa Mungu uliodhihirishwa kwao.
Hili ni tatizo kubwa kwa  kweli, Mara nyingi Mungu  amekuwa akiwapa upako, nguvu au uweza wa kufanya mambo  mbalimbali vijana. Sasa si vijana wote  wanaojua  namna  ya kushirikiana  na  huo upako ambao Mungu aliwapa kwa jambo fulani  Mfano, Mungu anaweza akampa kijana upako wa kuomba lakini  kijana  huyo badala ya kuomba yeye anaangalia  mpira, au ni mwanafunzi anatakiwa kusoma na Mungu ameleta upako  huo  sasa yeye anaenda kuomba mambo huwa hayakai hivyo. Upako lazima utumike kwa kusudi  lile  uliotumiwa. Upako wowote unaokuja kwako unakuja kwa kusudi maalumu. 
Nne Kukosa maarifa ya Mungu.
Mungu anasema katika Hosea 4:6 kila kipengele cha kwanza  watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa na pia katika Zaburi 119:9 anasema “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii akilifuata neno lake”. Sasa kwa sababu  nazungumza na vijana naweza nikaweka mistari huu hivi “Vijana wangu wanaagamizwa kwa kukosa maarifa. Maarifa yanayozungumzia hapa ni mafundisho ya neno la Mungu.
Vijana wengi wako  tayari kuangalia mechi mbili mfululizo kuanzia saa nne kasoro usiku hadi saa  nane kwa masaa ya Kitanzania, lakini hawako tayari kusoma Biblia kwa saa moja, wako tayari kuangalia “Movie” za kinigeria, au za kizungu hata masaa matatu (3) lakini si kuangalia na kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu. Na Biblia inasema Apendaye mafundisho hupenda maarifa. Sasa kwa vile vijana wengi hawapendi mafundisho ndiyo maana hawako kwenye kusudi la Mungu. 
Tano, vijana wengi bado wanaipenda dunia,
Mzee Yohana katika 1Yohana 2:15” Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia, mtu akiipena dunia kumpenda Baba  hakupo ndani yake”. Na pia  Daudi anasema katika Zaburi  1:1 Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki wala  kusimama katika njia ya wakosaji wala     hakuketi barazani pa wenye mzaha.Ni vijana wachache sana katika  kanisa la leo ambao wako tayari kujikana nafsi zao kwa ajili ya Mungu wengi wanapenda kupoteza muda kwa habari  zisizo za Msingi, wengi wanapenda mzaha na utani, ni vijana wachache  ambao wanaweza kuacha kuangalia mchezo kwenye TV, au  akakataa kwenda kutembea ufukweni kwa lengo  la kuomba, au kusoma Neno, ninachojaribu kusema hapa ni hiki, najua kila jambo lina wakati wake, lakini ni vijana wachache sana waliojizuia katika mambo ya mwili kwa ajili ya kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu.
Sita, Vijana wengi hawajazivaa silaha za vita.
 Waefeso 6:11 Vaeni Silaha zote za Mungu, mpate kuzipinga hila  za shetani.Viajana wengi wameshindwa kumshinda mwovu kwa sababu hawazajivaa silaha za vita. Wengine hawajui silaha za vita ni zipi? Lakini wengine wanajua lakini hawajazivaa. Ile sura ya sita ya waefeso 6:10-18 Paulo anazungumzia silaha za vita, ambazo ni kwlei, haki, amani, Imani, wokovu na Neno la Mungu. Sasa hizi ni silaha na kama ni silaha zina namna zinavyovaliwa na namna zinavyotumika. Sasa si vijana wote waliozivaa silaha, wengi hawasomi neno la Mungu, hawatendi haki, wengi wana imani ya maneno isiyo ya  Matendo.
Saba, Vijana wengi wanaishi bila kuwa na malengo katika maisha yao / maono.
Mithali 29:18. Inasema “Pasipo maono watu huacha kujizuia bali ana heri mtu yule aishikaye sheria”. Hivi leo  ukiwauliza vijana wengi kwamba una maono au hasa malengo gani katika maisha yako? Asilimia kubwa watakujibu  sina malengo  yeyote  yale.Wakati huo huo hakuna aliyeumbwa kwa bahati mbaya Yeremia  29 :12. Kwa kila mtu Mungu analokusudi maalum la kumuumba na pia anayo malengo na mikakati ya kumpa huyu mtu atekeleze katika maisha yake. Sasa kwa sababu vijana wengi  hawana na hawajajua  hayo malengo ndio maana wanafanya  kila kinachotokea mbele yao bila kujua  kama ni kusudi la Mungu.
    Naamini  baada ya kuwa umesoma ujumbe huu umepata maarifa ya kukusaidia kukaa katika nafasi yako kama kijana kwa sababu umeshajua sababu za kuktokukaa kwenye nafasi yako.

Friday, April 20, 2012

IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 3)



IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 3)

(Umuhimu wa taarifa na mahusiano mazuri baina ya mlinzi na watu wa eneo lake)
Na: Patrick Sanga
Katika sehemu ya pili naliahidi kwamba ningeanza kuelezea kuhusu nafasi mbalimbali za ulinzi, lakini ndani yangu nimesikia kuandika mambo kadhaa yafuatayo tena kabla sijaanza kuandika kwa habari ya nafasi husika. Ni imani yangu kwamba sehemu ya nne itaanza kwa kuelezea nafasi husika, fuatana nami tuendeleae.
Jambo ambalo nimesukumwa niandike kwa habari ya eneo hili la tatu ni umuhimu wa taarifa na mahusiano mazuri baina ya mlinzi na watu wa eneo lake.
Jambo la kwaza – Umuhimu wa taarifa ya mlinzi kwa watu wa eneo lake
Hebu tuangalie jambo hili kupitia kitabu cha Mathayo 25:1-13. Hii ni habari ya wanawali kumi waliokuwa wakimsubiri Bwana Harusi. Biblia inatuambia watano kati yao walikuwa na busara na watano walikuwa wapumbavu. Busara ya wale watano wa kwanza ni kuwa na taa zenye mafuta ya akiba huku wakimsubiri Bwana, na upumbavu wa wale watano wengine ni kuwa na taa zisizo na mafuta ya akiba huku wakimngoja Bwana harusi pia.
Kwa sababu ya Bwana harusi kuchelewa wanawali hawa wote waliamua kulala. Ule mstari wa sita na saba inasema ‘Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, Bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao’.
Katika sehemu ya pili ya somo hili niliandika kwamba jifunze kuitazama taarifa ya mlinzi kama fursa ya matengenezo. Biblia iko wazi kwamba wanawali hawa waliamua kulala baada ya kuona Bwana harusi wao amechelewa. Kumbuka kwamba lengo la wote hawa ilikuwa ni kumlaki Bwana Harusi. Sasa kilichowaamsha toka usingizini ni ‘kelele za taarifa’ ambazo ninaamini zilikuwa za walinzi ambao jukumu lao ilikuwa ni kutoa taarifa juu ya uwepo au ujio wa Bwana harusi husika.
Kutokana na mfano huu tunajifunza kwamba mosi taarifa ya mlinzi/walinzi iliwasaidia wanawali kuamka kutoka usingizini maana walikuwa wamelala. Licha ya taarifa kuwasiaida kuamka usingizini, taarifa ya mlinzi ilitoa fursa ya wanawali kujiandaa. Tumeona katika mstari wa saba kwamba punde baada ya taarifa wale wanawali wakaamka na kuziandaa/zitengeneza taa zao. Naam taarifa ya walinzi ilitoa fursa ya matengenezo. Hivyo hata sasa Mungu anapoleta taarifa kwako, ujue analeta taarifa ya matengenezo, naam mbele kuna jambo linakuja, hivyo analeta taarifa mapema kupitia walinzi wako au wa eneo lako ili uitumie kutenda yapasayo. 
Jambo la pili – Umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri kati ya Mlinzi na watu wa eneo lake.
Kupitia mfano huu wa wanawali kumi tunagundua pia kwamba, taarifa ya mlinzi ilitoa fursa ya mawasiliano baina yao. Kabla ya taarifa hatuoni wanawali hawa wakiwasiliana kwa jambo lolote. Si hivyo bali pia tunagundua kwamba baada ya taarifa ya mlinzi ndipo fahamu za wale wanawali wapumbavu zikafunguka na wakajua mafuta yao hayatoshelezi. Kwa mujibu wa Biblia harusini aliruhusiwa kuingia mtu (mwanamwali) mwenye taa inayowaka yaani taa yenye mafuta.
Je, ni kwa nini wale wanawali wapumbavu kabla hawajaenda kulala hawakufikiri kwamba mafuta haya yakiisha na hatuna ya akiba hatuwezi kuingia harusini?  Huenda hawakujua kwamba mwanamwali mwenye taa inayowaka ndiye atakayeruhusiwa kuingia harusini. Jambo ninalotaka ulione ni kwamba pamoja na kutokujua kwao, walinzi wa mji walijua nini kinatakiwa kwa mtu kuingia harusini. Laiti wanawali wangekuwa na mahusiano mazuri na walinzi wa mji wangepewa siri kuhusu ujio wa Bwana harusi wao. Lakini kwa sababu hawakuwa na mahusiano mazuri na walinzi, walishindwa kuwauliza wale walinzi mahitaji ya msingi atakapokuaja Bwana harusi. Naam wakajikuta wameachwa na Bwana wao walipoenda kutafuta mafuta. 
Ukweli huu kuhusu mahusiano unathibitishwa katika kitabu cha Wimbo Ulio Bora 3:3 unaosema ‘Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu’. Habari hii inatueleza habari za kijana aliyekuwa anamtafuta mwenza (mpenzi) wake kwa muda mrefu bila mafanikio. Katika kuendelea kumtafuta ndipo akakutana na walinzi wa mji, akawauliza mmemwona mpendwa wa nafsi yangu?          Ni imani yangu walinzi wale walimjibu, kwa sababu mstari wa nne unatumabia ‘kitambo kidogo tu nikishakuwaondokea, nikamwona mpendwa wa nafsi yangu, Nikamshika nisimwache tena…’ Hivyo ufumbuzi wa tatizo (hitaji) la huyu kijana ulipatikana kwa walinzi wa mji. Kwa hakika mahusiano mazuri ya Walinzi na yule kijana yalipelekea hitaji la kijana kufanikiwa au kufikiwa.
Kutokana na habari hii ni dhahiri kwamba walinzi wamewekwa kwenye nafasi zao ili kuleta ufumbuzi juu ya changamoto zinazomkabili mwanadamu kwa kumjulisha mawazo ya Mungu juu yake, ili pia kumsaidia mwanandamu aishi kwa kulitumikia shauri la Mungu katika siku zake. Biblia katika kitabu cha Isaya 62:6-7 inasema  ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’.
Mungu anataka yawepo mawasiliano na mahusiano mazuri kati ya Mlinzi (Walinzi) na wanaolindwa. Katika andiko hilo hapo juu, licha ya Mungu kuweka walinzi juu ya kuta za Yerusalemu ilibidi awape taarifa na wakazi wa mji huo, ili wasije, walinzi hao wakatoa taarifa ya kile Mungu amesema na wakazi wa Yesrusalemu wakapuuza, mwisho wao wakaangamia.
Ukisoma pia Biblia katika kitabu cha Mathayo 24:43 inasema ‘Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angalijua ile zamu mwivi atakayokuja, anagalikesha, wala asingeliacha nyumba yake kuvunjwa’. Naam kiroho milinzi au walinzi ndio waliopewa uwezo wa kuona nini kinakuja juu yako, ndoa yako, kazi yako, huduma yako, taifa lako nk. Kwa sababu hii ni muhimu sana kuwa na mahusiano mazuri na mlinzi au walinzi ambao Bwana Mungu amekuweka chini ya Mlango au Himaya yao. Naam kufanikiwa kwa kazi ya mlinzi katika nafasi yake kunategemea mahusiano na ushirikiano anaopata kutoka kwa watu wa eneo lake.   
Mungu akubariki kwa kufuatilia mfululizo huu, usiache kuombea muendelezo wa somo hili. Tutaendelea na sehemu ya nne…

NAFASI YA MWANAMKE KIBIBLIA.

kllk


NAFASI YA MWANAMKE KIBIBLIA.

Na; Patrick samson Sanga.
Mwanzo 1:27 ‘Mungu akaumba mtu kwa mfano wake,kwa mfano wa Mungu alimwumba,mwanaume na mwanamke aliwaumba. Sikiliza mahali popote pale mwanamke ni mtu mwenye nguvu na ushawishi mkubwa katika kufanya mambo kuliko hata mwanaume.Ikiwa ushawishi huu utatumiwa katika mpango wa Mungu basi kusudi la Mungu litatekelezwa.
Mungu hakumwumba mwanamke kwa bahati mbaya au makosa,kila ambacho Mungu alikifanya ,alikifanya kwa kusudi.kwa lugha nyingine kila ambacho Mungu alikifanya maana yake moja kina nafasi mbele zake na mbili kuna wajibu ambao Mungu aliweka ili utekelezwe na hicho kitu.
Lengo la ujumbe huu ni kukueleza nafasi ambayo Mungu amempa mwanamke katika kanisa,jamii,nchi,ndoa na nk na wajibu wa yeye kutekeleza katika nafasi hiyo:-
1.Mungu anamtazama mwanamke kama msaidizi wa mumewe . Mwanzo 2:18 “Bwana Mungu akasema si vyema huyo mtu awe peke yake,nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye”. Tangu kuumbwa kwa Adam,mpaka Mungu kumletea Eva inasemekana miaka mingi ilipita hapa katikati.Sasa tunajua katika ile sura ya kwanza na ya pili ya kitabu cha mwanzo,Mungu alikuwa amempa Adam wajibu wa kutekeleza.
Ikafika wakati Mungu akaona ule wajibu ni mkubwa sana kwa Adam kuutekelekeza ndipo akampa Eva.Kitu Mungu anataka tujue hapa ni hiki,wajibu aliopewa Adam peke yake asingeweza kuutekeleza bila Eva,maana yake nafasi ya Eva kwa Adam ilikuwa ni ya muhimu zaidi.Pasipo Eva,Adam angeshindwa kutekeleza wajibu.
Sasa hata leo katika ndoa,kanisa Mungu ameweka wanawake ili wawe wasaidizi katika majukumu ambayo Mungu amewapa na waume zao au wachungaji wao makanisani.
2. Mwanamke kama mlinzi wa agano na kusudi la Mungu. Mithali 14:1 “ Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake ; bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe” , Mwanzo 3;13 “ Bwana Mungu akamwambia mwanamke ,nini hili ulilolifanya ? Mwanamke akasema nyoka alinidanganya ,nikala”..
Ndoa ni agano la Mungu kwa wanadamu. Mlinzi wa agano kimsingi ni mwanamke. Mara nyingi shetani akitaka kuvuruga ndoa atatafuta mpenyo au nafasi hiyo kwa mwanamke ili asambaratishe ndoa hiyo.Sasa mwanamke yupo ili kulinda kusudi hilo.Asipokaa kwenye nafasi yake ya ulinzi basi ajue kwamba kusudi la Mungu la kuwaunganisha halitatimia.
Nisikilize ndoa yoyote inapovuruguka ujue mwanamke hakusimama vema kwenye nafasi yake ya ulinzi. Ngoja nikuonyeshe kitu hiki. Adam na Eva walipokula tunda ambalo Mungu aliwaambia wasile , kila mmoja wao aliulwiza swali lake. Adamu aliulizwa uko wapi? Mwanzo 3:9, na Eva alimwambia Mwanamke ni nini hili ulilolifanya , Mwanzo 3:13.Ipo tofauti kubwa sana katika haya maswali mawili.Swali la Adam lilimaanisha kwa nini haupo kwenye nafasi yako? Na swali la Eva lilivuka hapo na kumaanisha kwa nini hujafanya ulilotakiwa kufanya yaani kulinda agano.Mahali popote mwanamke ulipo ikiwa ni katika ndoa ,kanisa ,jamii,nchi, jifunze kulinda kusudi la Mungu ambalo unajua Mungu amekuagiza . jifunze kupitia mama yake Musa , yeye alilinda agano la wana wa wa Israeli kwa kumficha Musa na kuhakikisha hafi maana alijua Musa hakuzaliwa kwa bahati mbaya. Kutoka 2:1-10.

3.mwanamke kama muombolezaji.
Luka 23;27-28 “Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata na wanawake waliokuwa wakijipiga vifiua na kumuombolezea , Yesu akawageukia akasema ,Enyi binti za Yerusalemu ,msinillie mimi bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu”.Sikliliza , Mungu amweapa kinamama uwezo mkubwa wa kuomboleza kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ndani ya jamii ,ndoa, kanisa, nchi nk. Hivyo Mungu anamuhesabu mwanamke kama muombolezaji.
Hii ina maana kam kuna vitu havijakaa sawasawa kwenye ndoa,kanisa,nchi nk, Mungu anajua mwanamke atasimama kwenye nafasi yake na kuomba ili Mungu apate kuliponya taifa kupitia maombi .Ukiona maasi mengi yamezidi katika taifa mfano, vijana wa kike kutoa mimba, uasherati,uchafu na uzinzi basi ujue kina mama katika mji au taifa hawajasimama vizuri kwenye nafasi zao. Si kana kwamba nawalaaumu mama zangu na dada zangu kwa kusema hivyo,bali ninachotaka niwaonyeshe ni kwamba usalama na maendeleo mazuri ya vijana wa kike na kiume katika familia,kanisa na taifa kwa ujumla upo katika mikono yenu na ndio maana Yesu aliwaambia mjililie ninyi na hao vijana wenu.
Nikuulize swali , jiulize una weatoto wangapi? Tabia na mwenendo wao ukoje? Je ni mzuri? Unambariki Mungu? sivyo jiulize chanzo cha tabia hizo kwa mwananao ni nini au ni nani aliyehusika na tabia hiyo? Najua unaweza kwa haraka kusema ni shetani au kumtupia lawama mmeo. Sikiliza Shatani huwa hafanyi chochote isipokuwa pale anapokuwa  amepewa nafasi na mtu au watu fulani , kwa kifupi mtu anaposhindwa kusimama kwenye nafasi yake. Sasa ukisoma vizuri Biblia utagundua nafasi ambayo Mungu amempa  mwanamke kwa habari ya watoto wake, ndoa yake, kanisa lake kwa ujumla.
Jifunze kusimama kwenye nafasi yako, funga na kuomba kwa ajili ya taifa hili ili Bwana Mungu apate kuliponya . maombi yako yatasababisha kutengenezwa kwa mahali palipobomoka na krejeshwa kwa njia za kukalia.
4.Mwanamke kama mlinzi wa nafsi ya mtoto wake wa kiume .
Katika hii sura ya 31 ya kitabu cha Mithali tunaona habari za mama mmoja ambaye alikuwa na mtoto wa kiume na huyu mtoto alikuwa ni mfalme. Ule mstari wa pili unasema “ Ni nini mwanangu ?, tena ,nini mwana wa tumbo langu? Tena nini mwana wa nadhiri zangu ? Usiwape wanawake nguvu zako; wala moyo wako usiwape wale waharibuo wafalme”. kinamama wakijua namna ya kuzikamata nafsi za watoto wao wa kiume ,nakuambia kuna uwezekano mkubwa kabisa hawa watoto wasifanye tendo la ndoa mpaka watakapo kuja kuoa.
Hili litawezekana pale tu kinamama watapofanikiwa kuzikamata na kukaa kwenye nafsi za watoto wao wa kiume.Huyu mama alimuuliza maswali mengi mwanawe kwa sababu aliona nafasi yake mama kwenye nafsi ya mwanawe inanyang’anywa na wanawake wengine.
Naamini waraka huu mfupi na wa kwanza utafanyika kuwa msaada kwa wamama wengi mahala popote pale.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.

ENYI WANAWAKE MSINILILIE MIMI.


ENYI WANAWAKE MSINILILIE MIMI.

 Na; Patrick Samson Sanga.
Kwa nini Yesu aliwaambia akinamama jililieni nafsi zenu na watoto wenu ?
Luka 23:27-28 “Na mkutano mkubwa wa watu wakamfuata na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea, Yesu akawageukia,akasema,Enyi binti za Yerusalemu ,msinililie mimi,bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu”.
Hapa Bwana wetu Yesu alikuwa njiani kuelekea Golgotha kusulubiwa, akina mama na binti za Yerusalemu wakawa wanamlilia na kumwombolezea Yesu kwa uchungu sana.
Sasa kwa kawaida mtu anapokuwa anapita kwenye hali ngumu au matatizo au msiba au janga lolote zito kwa kawaida tunapenda watu wengine watufariji na waomboleze pamoja na sisi na ndiyo maana hata Paulo alisema lieni pamoja na wanao lia nk
Lakini jambo hili halikuwa hivyo kwa Yesu ,kile kilio cha wale akina mama kilimfanya Yesu awageukie na kutoa ujumbe wa ajabu kwa wale akina mama na ndipo akasema msinililie mimi,bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu .
Nimeandika ujumbe huu mfupi ili kujibu maswali mawili ambayo tunayapata kutoka katika sentensi ya Bwana wetu Yesu kwa hawa wamama nayo ni;
Moja, kwa nini Yesu aliwaambia msinililie mimi ? mbili kwa nini Yesu aliwaambia jililieni nafsi zenu na watoto wenu?. Yesu aliwaambia msinililie mimi kuu mbili nazo ni;
{a}Ili neno liweze kutimia.Yohana 3:16. Mapatano ya Yesu na baba kule mbinguni ilikuwa Yesu aje na afe  kwa ajili ya watu wake. Ili mlazimu Yesu kupita kwenye hiyo njia, hata kama wangeombolezaje kilio chao kisingeweza zuia kifo cha Bwana Yesu.
Kumbuka kule Gethsemane Ysu mwenyewe aliomba akasema Baba, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, Lakini tunaona Mungu alituma malaika kumfariji na kumtia moyo na Yesu mwenyewe alikuwa tayari mapenzi ya Mungu yatimizwe.
{b} Kilio chao kingemhuzunisha na kumvunja moyo zaidi. Matendo ya Mitume 21:9-14.Hapa ulikuwa umetolewa unabii wa jinsi vile Paulo atakavyouawa kule Yerusalemu. Na watu wa nyumba ile wakaanza kulia na kumsihi Paulo asipande kwenda Yerusalemu, Ndipo Paulo akawaambia mnafanya nnini, kulia na kunivunja moyo?. Kwa hiyo hata Yesu angekutana na hali ka,a ya Paulo.
Swali la pili; Kwa nini Yesu aliwaambia wamama bali jililieni nafsi zenu na wato wenu na Je alikuwa ana maana gain kuwaambia hivyo?
 Kabla sijakuambia hizo sababu, ngoja kwa kifupi nikuambie habari za nafsi. Kwa kiyunani inaitwa (psuche).Nafsi inahusika kuelekea ndani ya mtu.Ndani ya nafsi ndiko kwenye hisia,akili na maamuzi ya mtu.Hivyo nafsi ya mtu inahusika na maauzi, hisia na nia za mtu binafsi. Nafsi inatabia ya kuugua,kuinama, na na kuumia pale inapojeruhiwa.
Siku zote nafsi inagojea mwongozo wa roho au mwili wa mtu. Mtu akiwa ni wa rohoni nafsi itakaa mkao wa rohoni na mtu akiwa ni wa mwilini na nafsi yake itakaa mkao wa mwilini.Nafsi inaishi sasa kwa kutegemea maneneo unayojisemea au kusemewa na wengine sasa au wakati uliopita.Hivyo Yesu alipowaambia wale kinamama msinililie mimi alikuwa na maana hii na sababu hizi;
*Moja, Yesu alijua akinamama wengi ni watu ambao nafsi zao ni rahisi kujeruhika na kuinama pindi wanapokutana na matatizo mbalimbali na zaidi kina mama wengi ni watu ambao ni wepesi sana kuijtamkia maneno ambayo kwa namna moja au nyingine yanajeruhi nafsi na kuharibu future yao wenyewe.
Kwa Kujua kwamba akina mama wengi mara nyingi huwa wanajitamkia maneno ambayo yanaathari kwao wenyewe, watoto wao, familia zao, kanisa lao na hata nchi nk ndio maana Yesu alisema jililieni nafsi zenu.
 Alikuwa akimaanisha nini?
Yesu alikuwa anawaambia wale wamama wajitunze nafsi zao na za watoto wao kwa kuhakikisha ndani wanweka neno la Mungu linalozungumzia maisha yao ya baadae (future).
Hili neno litazifanya hisia zao, na akili zao na maamuzi yawe yatawaliwe na ahadi za Mungu na hii itawasaidia nafsi kutokuinama wala kujeruhika pindi wanapokutana na matatizo mbalimbali. Neno hili litawapa jibu la kukabiliana na mazingira ya kila nmana kwa sababu hiyo Jehanamu itakosa watu .
*Mbili ni kwa sababu ya nafasi na wajibu ambao Mungu amewapa akinamama kama walinzi wa kusudi lake popote pale walipo.
Nisikilize mwanamke Mungu amekuheshimu sana kukupa wajibu wa kulinda agano na kusudi lake duniani.Shetani anapotaka kuvuruga na kuharibu kusudi la Mungu mahali popote pale, uwe na uhakika lazima tu ataanza kutafuta njia na mpenyo kwa mwanamke.Shetani akitaka kuleta vurugu kwenye ndoa,kanisa,familia uwe na uhakika atafanya kila analoweza apitie kwa mwanamke.
Hebu chukua dakika moja tafakari vile shetani anavyovuruga vijana wa kike na wa kiume, kwa kuwafanya mabinti watoe mimba na kuua bila hata hofu kwa Mungu, Wazazi kufanya tendo la ndoa na wanao, ndugu kwa ndugu, Yesu aliona huzuni na kilio kikubwa ambacho kwanza kitawapata kinamama hapahapa duniani na baadaye katika dhiki kuu na mwisho katika Jehnamu ya moto na ndiyo maana alisema watasema heri wa matumbo yasiyozaa na matiti yasiyonyonyesha.
Mwanamke hakikisha uniombolozea nafsi na kuiambia nafsi yangu mtii Mungu, nafsi yangu usiiname kwa yale unayoaona, hawa watoto wangu si ya dunia, iambie nafsi yako kwamba hawa watoto, hii ndoa, kanisa, vijana,nchi nk ni ya Bwana .
Hakuna hata mmoja wa watoto wangu watakaokwenda Jehnamu , sizai watoto wa kwenda Jehanamu nk.Hakikisha ndani yako ahadi za Mungu zinajaa kwa wingi ili nafsi isitekwe na hivyo ukawa umemruhusu shetani kuvuruga na kuharibu kusudi la Mungu kupitia wewe .
Naamini ujumbe huu utawasidia wamama wengi Kujua namna ya kushughulika na nafsi zao na kuhakikihsa haziwafanyi kutoka kwenye kusudi la Mungu.
Neema ya Kristo na iwe nawe.

MWANAMKE, JIFUNZE KUSIMAMA KWENYE NAFASI YAKO KAMA MLINZI.


MWANAMKE, JIFUNZE KUSIMAMA KWENYE NAFASI YAKO KAMA MLINZI.


Na : Mwalimu Sanga P.S

Yeremia 31:22” hata lini utatanga tanga , Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani, mwanamke atamlinda mwanaume”.
Soma pia habari hii yote katika Isaya 32:9-17

Ule mstari wa tisa unasema “Inukeni enyi wanawake wenye raha, sikieni sauti yangu; enyi binti za watu wasiokuwa na uangalifu,tegeni masikio yenu msikie sauti yangu”.

Moja ya majukumu makubwa ambayo Mungu amemkabdihi mwanamke ni jukumu la ulinzi kwa mwamamumue yoyote na si mumewe tu kama wengi wanavodhani au kufikiri. Kwa maana hili andiko linawahusu wanwake haijalishi wameolewa au la, ni binti au mjane linamhusu.

Si wanawake wengi wanaoifahamu siri hii juu yao. Imeandikwa ya kwamba Mungu ameumba jambo jipya, mwanamke atamlinda mwanaume. Hii ina maana ulinzi wa mwanaume uko kwa mwanamke. Hii inaashiria kumbe Mungu ameweka neno la ulinzi wa mwanaume kwa mwanamke.

Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

*      Kuzaliwa kwa Musa, Kutoka 2;1-10.
Tunaona wazi kabisa mama wa Musa alivyomlinda mwanae akijua ndani yake kuna kusudi limebebwa.
*      Kuzaliwa, kukua na ndoa ya yakobo, Mwanzo 25:21-28, 27:1-4, 5, 6, 11-13, 17, 46.
Siri ya kusudi la Mungu hapa duniani kupitia Yakobo aliiweka kwa mamaye. Alimweleza maana ya vita iliyokuwa ikiendelea tumboni mwake alipokuwa mjamzito. Rebeka alihakikisha kusudi la Mungu juu ya watoto atakaowazaa linatimia, kwa sababu alijua Yakobo ndiye taifa kuu alihakikisha hilo linatimia na pia alihakikisha Yakobo haoi nje ya mpango wa Mungu kwa maana ya kuoa mataifa.
*      Kuzaliwa na maisha ya Samson, waamuzi 13:2-5, 12-15.
Siri ya nini Mungu amekiweka kwa Samson na kwa nini anamleta duniani, pamoja na namna mtoto huyo anavyotakiwa kulelewa aliiweka kwa mamaye Samson na si baba yake, Mzee Manoa. Sasa ukisoma utaona jinsi huyu mama alivyosimama kwenye nafasi yake ki ulinzi mpaka Samson alipoanza wajibu wake uliomleta duniani.
*      Zaidi unaweza ukajifunza pia kupitia kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Siri ya kitu gani kitazaliwa, Malaika aliileta kwa Mariam, akijua ni jukumu lake kulinda hiyo siri mpaka utimilifu wake. Soma Mathayo 1:18-25.

Hata leo wanawake wanatakiwa kusimama kwenye nafasi zao za ulinzi kwa ajili ya watoto wao, vijana wao, waume zao, ndugu zao waume nk. Kwa lugha nyepesi ni shauri la Bwana kwamba kila mwanamke amlinde mwanamume anayetoka katika tumbo lake, mumuwe kama ameolewa nk ili kuhakikisha kusudi la Mungu linatimia.

Kosa la hawa wanawake/mabinti katika siku za nabii Isaya ni kujisahau, kufurahia starehe na kutokuwa waangalifu katika kufuatilia maagizo ya Mungu kuhusu ulinzi wa watoto, vijana, na waume zao nk.

Kibiblia ni utaratibu wa Mungu kumpa kila mwanamke taarifa juu ya mtoto atayemzaa, juu ya mume ambaye atamuoa lengo ikiwa ni kumsaidia ajipange ki-ulinzi.

Mwanamke hakikisha unasimama vema kwenye nafasi yako ya ulinzi kwa mwanamume. Kama utasiamama vizuri kwenye nafasi yako ya ulinzi basi uwe na uhakika umeubariki moyo wa Mungu na kwa sababu hiyo umepelekea uponyaji kwenye familia yako, jamii yako, taifa lako na uchumi wako binafsi lakini na ule wa taifa pia.

Kazi kubwa ya Shetani ni kuwafanya wanawake waliokoka  duniani wajisahau, wasiwe waangalifu na hivyo wasifuatilie maagizo ambayo Bwana Mungu ameweka ndani yao kuhusu waume zao, vijana, watoto na ndugu zao wa kiume ili  kusudi la Mungu lisifanikiwe. Sasa wewe usikubali shetani akuzidi maarifa, weka neno hili kwenye matendo utaona wazo la Mungu linatimia kwa kuwa MWANAMKE AMESIMAMA KWENYE NAFASI YAKE YA ULINZI.

Bwana na akubariki.

MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO



MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO

Na: Patrick Sanga
Namshukuru Mungu ambaye anazidi kunipa neema ya kuandika na kuandika masomo mbalimbali na pia yale yanayohusu akina mama hasa wao kuwa kwenye nafasi zao.
Mnamo Novemba, 2009 mama mmoja alinitumia email akinieleza kwa jinsi ambavyo ndoa yake imekuwa ikimsumbua na kufika mahali pa yeye kujutia hata kwa nini alikubali kuolewa. Baada ya kupata ujumbe wake nilichukua hatua ya kufanya maombi kwa ajili ya huyu mama na wengine wenye shida kama yake kwenye ndoa zao. Katika kuomba, Mungu alinisemesha na kunifundisha kupitia Biblia mambo ya msingi ambayo sasa nimeona ni vema nikayaandaa kama somo na kuweka kwenye blog ili kila nafsi ya mwanamke yenye kuhitaji haya maarifa iweze kuyapata, maana imeandikwa katika Mithali 19:2 kwamba ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa’.
Mambo manne yafuatayo kama ukiyaweka kwenye matendo nina uhakika yataleta mabadiliko/uponyaji na pia kujenga msingi imara wa ndoa yako. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;
  • Sharti wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao.
Hili lilikuwa jambo la kwanza Bwana kunijulisha, ili niwakumbushe tena akina mama. Nimeshaandika kuhusu nafasi za Mwanamke huko nyuma, kwa ufafanuzi zaidi bonyeza link hii http://sanga.wordpress.com/2006/10/23/wanawake/. Kwa kifupi niseme uponyaji wa wa ndoa yako upo kwa wewe kuwa kwenye nafasi yako. Mungu hana namna ya kukusaidia kama hauko kwenye nafasi yako.
Ni lazima uzijue nafasi ambazo Mungu amekupa na kisha kusimama vema ukiwajibika kwenye hizo nafasi. Kinamama wengi leo wanalia sana Mungu aponye ndoa zao na matokeo yake yanakuwa tofauti na matarajio yao. Endapo kama na ndoa yako ipo kwenye eneo kama hili, angalia kama umekaa vizuri kwenye nafsi ambazo Mungu amkupa katika ulimwengu wa roho. Nina uhakika unaweza ukawa kuna maeneo ulijisahau hivyo tengeneza, maana uponyaji na uharibifu wa ndoa yako kimaandiko upo katika uwezo wako mama.
Ni maombi yangu kwamba Roho Mtakatifu akujulishe jambo hili, uponyaji wa ndoa yako haupo kwa Mungu, bali Mungu ameweka uwezo huo ndani yako. Ili uwezo huo uweze kufanya kazi sawasawa ni jukumu lako kuwa kwenye nafasi zako.  
  • Unahitaji hekima ya Mungu ili kujenga ndoa yako
Ukisoma kitabu cha Mithali 14:1 Biblia inasema “Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”. Biblia imeshaweka wazi kwamba wewe unaweza kuijenga au kuibomoa nyumba yako. Uwezo wa kufanya jambo hili unategemea kiwango cha hekima ya Mungu ambayo ipo ndani yako na juu yako pia. Hekima ya kuponya ndoa yako ambayo sasa unajua iko mashakani, ipo kwenye neno la Mungu na si kwa waganga wa kienyeji.
Unaipataje hekima ya Mungu?
Katika Mithali 8:1 Biblia inasema ‘Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?’ mstari wa 10 unasema ‘Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi’. Ule mstari wa 14 unasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi ni nguvu’. Na ule wa 16 unasema ‘Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’.
Siku zote kama unataka hekima ya Mungu ya kukusaidia kwenye eneo lolote la maisha yako utaipata kwenye neno la Mungu au kwa Mungu.  Imeandikwa katika Mithali 12:1a “Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Hekima ya Mungu kwa mtu ni matokeo ya kiwango cha neno la Mungu ambalo mtu ameliweka na kulitafakari kwa wingi moyoni mwake. Kwa hiyo kwa Watawala, hekima ya Mungu kwa Mtawala inategemea kiwango cha neno la Mungu kuhusu utawala ambalo Mtawala amekiweka ndani yake. Naam hekima ya Mungu kwa Mwanamke itategema kiwango cha neno la Mungu kuhusu nafasi zako ambacho umekiweka ndani yao nk.
Sharti neno la Mungu kuhusu nafasi zako, wajibu wako nk liwe kwa wingi ndani yako ndipo hekima ya Mungu ya  kujenga nyumba/ndoa/familia yako itakapokaa ndani yako na juu yako. Na kwa kuwa hekima ni ufahamu, maarifa, shauri na nguvu, itakusaidia katika kuijenga ndoa yako, kama inavyowasaidia watawala, waung’wana na waamuzi katika majukumu yao (Mithali 8:16). Naam hekima hiyo itaongoza kinywa chako kuleta uponyaji wa ndoa na nyumba yako, kama Biblia inavyosema katika Mithali 31:26 “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake”.
Mithali 8:17 inasema ‘nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’. Naam siku zote, hekima inawasiaidia wale wanaoitafuta na wakaipata’. Na njia kubwa ya kupata hekima hiyo ni kwa njia ya kusoma na kuatafakari neno la Mungu kila siku na kuomba kama nilivyokufundisha hapo juu.
  • Uwe makini kufuatilia maisha ya mume wako/watu wa nyumbani mwako
Mithali 31: 27 “Huangalaia sana njia za watu wa nyumbani mwake; wala hali chakula cha uvivu”. Tafsiri ya kiingereza ya BBE inasemaShe gives attention to the ways of her family; she does not take her food without working for it”. Moja ya nafasi za mwanamke ambayo nilishaandika huko nyuma ni kuwa mlinzi wa mwanaume, hii ikiwa ni pamoja na mume wake.
Naam jukumu la ulinzi ni kubwa sana ambalo Mwanamke umepewa, siku zote mlinzi ana wajibu wa kufuatilia kwa karibu sana maisha/nyendo za yule  anayemlinda. Kwa dhana ya ndoa yako, ni jukumu lako kama mlinzi kufuatilia maisha ya mume wako na kujua kama anaishi katika mapenzi ya Mungu. Naam ukijua anaishi nje ya mapenzi ya Mungu simama kwenye nafasi zako uendelee kuomba huku ukiamini Mungu atambadilisha na kumsaidia kuishi katika mapenzi yake.
Kuwa makini kufuatilia maisha na njia za mume wako, itakusaidia kujua hali yake, na hatari ambayo inataka kumpata, hivyo kama mumeo ameokoka au ni mcha Mungu utakuwa na jukumu la kumtahadharisha kwamba awe makini na baadhi ya vitu ambavyo umeona asipokuwa makini navyo ataanguka. Naam kama hajaokoka na ni mtu ambaye hamjui wala kumjali Mungu, usikate tamaa na isikufanye ukaondoka kwenye nafasi yako, dumu hapo ukijua kwamba Mungu ni mwaminifu atafanya kwa kuzingtia maagizo yako kama mlinzi.
  • Usisubiri hadi tatizo litokee ndipo uanze kutafuta msaada wa Mungu
 Jifunze kutumia wakati wa amani kuweka msingi mzuri wa ulinzi kwenye ndoa yako. Usisubiri wakati wa hatari ndipo ujipange kwa mapambano. Ki Mungu kila siku kwako ni siku ya kujenga au kuongeza ukuta wa ulinzi kwa nyumba yako.   Sehemu kubwa ya maombi ambayo akina mama wanapeleka kwa Mungu ni ili apate kuziponya ndoa zao kwa sababu zimeingia kwenye matatizo. Sijui kama unaona jambo hili, wengi wanaomba kwa sababu ndoa zao zipo kwenye shida. Naam Mungu anataka ujifunze kuomba ulinzi wa ndoa yako wakati ndoa yako ina amani, tumia vizuri wakati wa amani kujenga kuta za ulinzi kwa ndoa na nyumba yako kwa ujumla.
 Ni imani yangu kwamba ujumbe huu, umekuongezea kwa kiasi fulani maarifa ya kukusaidia katika kuijenga ndoa yako. Jambo la msingi kujua ni kwamba, Katika kubadilisha maisha ya mume wako na kuiponya ndoa yako, Mungu anaangalia kwanza kama umesiamama kwenye nafasi zako na unatekeleza wajibu wako.
 Neema ya Kristo iwe nawe

JIFUNZE KUFIKIRI KABLA HUJACHUKUA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA


JIFUNZE KUFIKIRI KABLA HUJACHUKUA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA

Na: Patrick Samson Sanga
Nawasalimu kwa jina la Yesu . Leo katika nyanja hii ya vijana, nimeona ni vema tukashirikishana kuhusu suala la ‘kufikiri kabla ya kuoa au kuolewa’.
Siku moja katika kusoma Biblia nilikutana na mstari ufuatao, nakusahuri uusome kwa umakini. Biblia katika 1Wakorinto 7:8-9 inasema “Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.
Baada ya kuusoma mstari huu niliingia katika tafakuri nzito sana ambayo mwishowe ilinipeleka kuandaa somo hili, kwamba ni vema ukafikiri vizuri kabla ya kuchuka uamuzi wa kuoa au kuolewa.
Unajua malezi, dini, madhehebu yetu, wazazi, mila na desturi vinachangia kwa kiwango kikubwa sana kuhusu utaratibu wa kuanzia mtu kupata mke au mume mpaka watakapofunga ndoa. Kila kundi lina mfumo na utaratibu wake ambao lingependa vijana waufuate ili kuhakikisha wanaoa na kuolewa kwa kile ambacho kila kundi linaona na kuamini kwamba huo ndio uataratibu mzuri kufuatwa. 
Namshukuru Mungu kwa kuwa nami nimeoa, ingawa vitu vingi sana Bwana alikuwa ananifundisha vinavyohusu ndoa hata kabla sijaoa. Nakubaliana na dhana kwamba ili uweze kuwa Mwalimu mzuri kwenye nyanja fulani basi ni lazima au ni vema wewe mwenyewe ukawa umepitia kwanza kwenye nyanja hiyo. Lengo ikiwa sio tu ufundishe ‘theory’ bali pia utufundishe na uzoefu wako binafsi kwenye eneo hilo. Licha ya kukubaliana na dhana hii, kwangu binafsi haikuwa hivyo, maana kuna mambo mengi ambayo, Bwana Yesu, alikuwa ananifundisha yanayohusu ndoa hata kabla sijaoa.
Kwa kifupi ndoa ni shule au darasa ambalo wanandoa wanatakiwa kukaa chini na kujifunza kila siku namna ya kuishi humo ndani ili kuweza kuishi maisha ambayo Mungu amewakusudia.
Kutokana na mifumo ya baadhi ya makanisa yetu, si vijana wengi ambao wanafundishwa kwa undani kuhusu maamuzi haya makubwa. Wengi wao wameingia kimwili na kujikuta wakijutia na kulaumu kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu kijana. Nasema haya kwa kuwa nimekutana na wanandoa wengi wa aina hii, na nataka nikuambie kama Biblia ingetoa mwanya wa wanandoa kuachana na kuoa au kuolewa na mtu mwingine, wapendwa wengi sana walioko kwenye ndoa wangefanya hivyo na wengine wasingekubali kuolewa au kuoa tena.
Unajua kwa nini?
Ni kwa sababu si vijana wengi wenye ufahamu wa kutosha juu ya aina ya maamuzi wanayotaka kuyachukua. Kwa hiyo katika somo hili nimeona vema niandike mambo manne ya msingi ambayo naamini yataongeza na kupanua ufahamu wako ili kukusaidia kufikiri kwanza kabla ya kufanya maamuzi haya makubwa;
  • Si kila ndoa inayofungwa imeunganishwa na Mungu, kwa kuwa ndoa ni kiungo cha muhimu kwa Mungu na Shetani pia.
Kuanzia mwaka 2005, Mungu alinipa kibali cha kuanza kufundisha na pia kushauri  juu ya mambo kadhaa kuhusu wanandoa. Tangu wakati huo hadi sasa nimekutana na baadhi ya wanandoa ambao wanajuta kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Wanaishi kwenye ndoa kwa sababu tu ya watoto na pia kwa hofu kwamba endapo kama wataachana jamii na watu wanaowazunguka hawatawaelewa.
Ni vizuri ukafahamu kwamba si kila ndoa inayofungwa ni ya mapenzi ya Mungu, hata kama imefungwa kanisani. Biblia inaposema kilichounganishwa na Mungu, mwanadamu asikitenganishe, katika nafasi ya kwanza maana yake iwe ndoa ambayo Mungu ndiyo aliyehusika katika kuanzisha mahusiano na kuwaongoza hao watu kuishi pamoja. Wakati Mungu anatafuta kuhakikisha watu wake wanaoana katika mapenzi yake na Shetani naye anapambana kuhakikisha watu wanaoana katika hila (mapenzi) zake.
Shetani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kuvuruga wanandoa wengi na kuwafanya waishi maisha tofauti na yale ambayo Mungu aliwakusudia. Ni kwa sababu hii ndio maana Paulo aliwaambia Wakorinto ‘Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa’. Paulo aliona shida, maudhi ya wandugu walioko kwenye ndoa tokana na migogoro aliyokuwa akikutana nayo.
Fahamu kwamba ni furaha kubwa kwenye ufalme wa giza mtu anapooa au kuolewa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu Shetani anajua akifanikiwa kukushawishi ukaoa kinyume na mapenzi ya Mungu, ameharibu ‘future’ yako na kile ambacho Mungu alikusudia ukifanye hapa duniani. Kumbuka suala sio kuoa au kuolewa tu, bali ni kuingia kwenye ndoa ambayo itakuwezesha kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako. Hivyo kabla hujaamua nani uishi naye hakikisha unamshirikisha Mungu akuongoze kumpata mwenzi sahihi.
  • Unapaswa kuoa au kulewa katika mapenzi ya Mungu
Naam kuoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu ni changamoto nyingine kubwa kwa vijana wa kizazi cha leo. Naam hili ni eneo ambalo Mungu yupo makini sana kufuatilia nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Na upande wa pili nao, Shetani anapigana kwa juhudi kubwa ili kuvuruga kusudi la Mungu kupitia mtu au watu.
Ni vizuri ukafahamu kwamba unapotaka kufanya maamuzi ya kutaka kuoa au kuolewa, Shetani naye ataleta mawazo (mapenzi) yake ndani yako juu ya nani anafaa zaidi  kuwa mwenzi wako maisha. Lengo lake ni kuhakikisha anakuunganisha na mtu ambaye anajua kwa huyo atakumaliza kiroho na kihuduma kabisa. Suala sio kuwazuia msiende kanisani, bali ni kuhakikisha kile ambacho ungefanya kwa kuwa na mtu sahihi hakifanikiwi. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hili, muulize Mchungaji wako, kesi nyingi anazokutana nazo kanisani kwake zinahusu nini, naamini atakujibu kimapana. Ni jukumu lako kuwa makini kufuatilia unatii wazo la nani, Mungu au Shetani?  
  • Vigezo vya kimwili ni silaha kubwa ya uharibifu
Vigezo vya kimwili ni moja ya silaha kubwa ambazo Shetani anazitumia kuwavuruga watu wengi waweze kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu kwao. Jifunze kufukiri na kutafsiri mambo au makusudi kama Mungu anavyotazama na kutafsiri. Na uwezo wa kufanya hili utaupata kwenye neno lake tu. Kwako mwanaume Mungu anapokupa mke anakupa Mlinzi na msaidizi. Na kwa mwanamke Mungu anakuwa amekupa kichwa. Ni muhimu sana kuchunga ni msaidizi, mlinzi au kichwa gani unataka kiunganishwe na maisha yako kwa njia ya ndoa.
  • Ndoa ni wajibu mkubwa
Ndani ya ndoa kuna wajibu mkubwa sana unaokusubiri kama baba au mama. Ndani ya ndoa muda na uhuru wako unabanwa na mwenzi wako. Ndoa inabana pia muda wa kuwa na Mungu wako. Na kwa wengi kwa kutaka kuwapendeza zaidi waume au wake zao, wamefarakana na Mungu, kwa sababu wamewapa waume au wake zao hata nafasi na muda wa Mungu kwenye maisha yao.
Usiingie ndani ya ndoa kwa fikra za uapnde mmoja. Naam ndoa ni wito wa mapungufu na uvumilivu ambao ni lazima uwe tayari kuchukuliana na mwenzi wako katika mapungufu yake. Kuna vitu hamtaweza kufanana na kwa sababu ya mapungufu yaliyopo kwa kila mmoja  unapaswa kutafakari kuhusu majukumu yanayokuja kwako kama mwanandoa, hekima na busara katika kuzikabili changamoto za ndoa, kama vile kuzaa au kutokuzaa, kutokujiweza katika masuala ya unyumba, matumizi ya fedha, tabia za mwenzi wako nk.
Haya ni mambo ya kuhakikisha unayaombea mapema ili kujenga msingi imara utakapoingia kwenye ndoa yako. Lakini nikutie moyo kwamba endapo utaoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu, yeye ni mwaminifu, atakuunganisha na mtu ambaye katika changamoto mtakazokutana nazo hazitawakwamisha wala kuwafanya mjute. Bali endapo Shetani ndiye ataongoza maamuzi yako, ni majuto makubwa sana (asomaye na afahamu).
Mungu akubariki, naamini ujumbe huu umeongezea mambo ya kutafakari na kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi wa kuoa au kuolewa.