MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO
Namshukuru Mungu ambaye anazidi kunipa neema ya kuandika na kuandika
masomo mbalimbali na pia yale yanayohusu akina mama hasa wao kuwa kwenye
nafasi zao.
Mnamo Novemba, 2009 mama mmoja alinitumia email akinieleza kwa jinsi
ambavyo ndoa yake imekuwa ikimsumbua na kufika mahali pa yeye kujutia
hata kwa nini alikubali kuolewa. Baada ya kupata ujumbe wake nilichukua
hatua ya kufanya maombi kwa ajili ya huyu mama na wengine wenye shida
kama yake kwenye ndoa zao. Katika kuomba, Mungu alinisemesha na
kunifundisha kupitia Biblia mambo ya msingi ambayo sasa nimeona ni vema
nikayaandaa kama somo na kuweka kwenye blog ili kila nafsi ya mwanamke
yenye kuhitaji haya maarifa iweze kuyapata, maana imeandikwa katika
Mithali 19:2 kwamba ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa’.
Mambo manne yafuatayo kama ukiyaweka kwenye matendo nina uhakika
yataleta mabadiliko/uponyaji na pia kujenga msingi imara wa ndoa yako.
Mambo hayo ni kama ifuatavyo;
- Sharti wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao.
Hili lilikuwa jambo la kwanza Bwana kunijulisha, ili niwakumbushe
tena akina mama. Nimeshaandika kuhusu nafasi za Mwanamke huko nyuma, kwa
ufafanuzi zaidi bonyeza link hii http://sanga.wordpress.com/2006/10/23/wanawake/. Kwa kifupi niseme uponyaji wa wa ndoa yako upo kwa wewe kuwa kwenye nafasi yako. Mungu hana namna ya kukusaidia kama hauko kwenye nafasi yako.
Ni lazima uzijue nafasi ambazo Mungu amekupa na kisha kusimama vema
ukiwajibika kwenye hizo nafasi. Kinamama wengi leo wanalia sana Mungu
aponye ndoa zao na matokeo yake yanakuwa tofauti na matarajio yao.
Endapo kama na ndoa yako ipo kwenye eneo kama hili, angalia kama umekaa
vizuri kwenye nafsi ambazo Mungu amkupa katika ulimwengu wa roho. Nina
uhakika unaweza ukawa kuna maeneo ulijisahau hivyo tengeneza, maana
uponyaji na uharibifu wa ndoa yako kimaandiko upo katika uwezo wako
mama.
Ni maombi yangu kwamba Roho Mtakatifu akujulishe jambo hili, uponyaji
wa ndoa yako haupo kwa Mungu, bali Mungu ameweka uwezo huo ndani yako.
Ili uwezo huo uweze kufanya kazi sawasawa ni jukumu lako kuwa kwenye
nafasi zako.
- Unahitaji hekima ya Mungu ili kujenga ndoa yako
Ukisoma kitabu cha Mithali 14:1 Biblia inasema “Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”.
Biblia imeshaweka wazi kwamba wewe unaweza kuijenga au kuibomoa nyumba
yako. Uwezo wa kufanya jambo hili unategemea kiwango cha hekima ya Mungu
ambayo ipo ndani yako na juu yako pia. Hekima ya kuponya ndoa yako
ambayo sasa unajua iko mashakani, ipo kwenye neno la Mungu na si kwa
waganga wa kienyeji.
Unaipataje hekima ya Mungu?
Katika Mithali 8:1 Biblia inasema ‘Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?’ mstari wa 10 unasema ‘Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi’. Ule mstari wa 14 unasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi ni nguvu’. Na ule wa 16 unasema ‘Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’.
Siku zote kama unataka hekima ya Mungu ya kukusaidia kwenye eneo
lolote la maisha yako utaipata kwenye neno la Mungu au kwa Mungu.
Imeandikwa katika Mithali 12:1a “Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Hekima
ya Mungu kwa mtu ni matokeo ya kiwango cha neno la Mungu ambalo mtu
ameliweka na kulitafakari kwa wingi moyoni mwake. Kwa hiyo kwa Watawala,
hekima ya Mungu kwa Mtawala inategemea kiwango cha neno la Mungu kuhusu
utawala ambalo Mtawala amekiweka ndani yake. Naam hekima ya Mungu kwa
Mwanamke itategema kiwango cha neno la Mungu kuhusu nafasi zako ambacho
umekiweka ndani yao nk.
Sharti neno la Mungu kuhusu nafasi zako, wajibu wako nk liwe kwa
wingi ndani yako ndipo hekima ya Mungu ya kujenga nyumba/ndoa/familia
yako itakapokaa ndani yako na juu yako. Na kwa kuwa hekima ni ufahamu,
maarifa, shauri na nguvu, itakusaidia katika kuijenga ndoa yako, kama
inavyowasaidia watawala, waung’wana na waamuzi katika majukumu yao
(Mithali 8:16). Naam hekima hiyo itaongoza kinywa chako kuleta uponyaji
wa ndoa na nyumba yako, kama Biblia inavyosema katika Mithali 31:26 “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake”.
Mithali 8:17 inasema ‘nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’.
Naam siku zote, hekima inawasiaidia wale wanaoitafuta na wakaipata’. Na
njia kubwa ya kupata hekima hiyo ni kwa njia ya kusoma na kuatafakari
neno la Mungu kila siku na kuomba kama nilivyokufundisha hapo juu.
- Uwe makini kufuatilia maisha ya mume wako/watu wa nyumbani mwako
Mithali 31: 27 “Huangalaia sana njia za watu wa nyumbani mwake; wala hali chakula cha uvivu”. Tafsiri ya kiingereza ya BBE inasema “She gives attention to the ways of her family; she does not take her food without working for it”. Moja ya nafasi za mwanamke ambayo nilishaandika huko nyuma ni kuwa mlinzi wa mwanaume, hii ikiwa ni pamoja na mume wake.
Naam jukumu la ulinzi ni kubwa sana ambalo Mwanamke umepewa, siku zote mlinzi ana wajibu wa kufuatilia kwa karibu sana maisha/nyendo za yule anayemlinda.
Kwa dhana ya ndoa yako, ni jukumu lako kama mlinzi kufuatilia maisha ya
mume wako na kujua kama anaishi katika mapenzi ya Mungu. Naam ukijua
anaishi nje ya mapenzi ya Mungu simama kwenye nafasi zako uendelee
kuomba huku ukiamini Mungu atambadilisha na kumsaidia kuishi katika
mapenzi yake.
Kuwa makini kufuatilia maisha na njia za mume wako, itakusaidia kujua
hali yake, na hatari ambayo inataka kumpata, hivyo kama mumeo ameokoka
au ni mcha Mungu utakuwa na jukumu la kumtahadharisha kwamba awe makini
na baadhi ya vitu ambavyo umeona asipokuwa makini navyo ataanguka. Naam
kama hajaokoka na ni mtu ambaye hamjui wala kumjali Mungu, usikate tamaa
na isikufanye ukaondoka kwenye nafasi yako, dumu hapo ukijua kwamba
Mungu ni mwaminifu atafanya kwa kuzingtia maagizo yako kama mlinzi.
- Usisubiri hadi tatizo litokee ndipo uanze kutafuta msaada wa Mungu
Jifunze kutumia wakati wa amani kuweka msingi mzuri wa ulinzi kwenye
ndoa yako. Usisubiri wakati wa hatari ndipo ujipange kwa mapambano. Ki
Mungu kila siku kwako ni siku ya kujenga au kuongeza ukuta wa ulinzi kwa
nyumba yako. Sehemu kubwa ya maombi ambayo akina mama wanapeleka kwa
Mungu ni ili apate kuziponya ndoa zao kwa sababu zimeingia kwenye
matatizo. Sijui kama unaona jambo hili, wengi wanaomba kwa sababu ndoa
zao zipo kwenye shida. Naam Mungu anataka ujifunze kuomba ulinzi
wa ndoa yako wakati ndoa yako ina amani, tumia vizuri wakati wa amani
kujenga kuta za ulinzi kwa ndoa na nyumba yako kwa ujumla.
Ni imani yangu kwamba ujumbe huu, umekuongezea kwa kiasi fulani
maarifa ya kukusaidia katika kuijenga ndoa yako. Jambo la msingi kujua
ni kwamba, Katika kubadilisha maisha ya mume wako na kuiponya ndoa yako,
Mungu anaangalia kwanza kama umesiamama kwenye nafasi zako na
unatekeleza wajibu wako.
Neema ya Kristo iwe nawe
Edifying...be blest great man of God!!
ReplyDeleteEdifying...be blest great man of God!!
ReplyDeleteEdifying...be blest great man of God!!
ReplyDelete