Friday, April 20, 2012

IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 3)



IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO (Part 3)

(Umuhimu wa taarifa na mahusiano mazuri baina ya mlinzi na watu wa eneo lake)
Na: Patrick Sanga
Katika sehemu ya pili naliahidi kwamba ningeanza kuelezea kuhusu nafasi mbalimbali za ulinzi, lakini ndani yangu nimesikia kuandika mambo kadhaa yafuatayo tena kabla sijaanza kuandika kwa habari ya nafasi husika. Ni imani yangu kwamba sehemu ya nne itaanza kwa kuelezea nafasi husika, fuatana nami tuendeleae.
Jambo ambalo nimesukumwa niandike kwa habari ya eneo hili la tatu ni umuhimu wa taarifa na mahusiano mazuri baina ya mlinzi na watu wa eneo lake.
Jambo la kwaza – Umuhimu wa taarifa ya mlinzi kwa watu wa eneo lake
Hebu tuangalie jambo hili kupitia kitabu cha Mathayo 25:1-13. Hii ni habari ya wanawali kumi waliokuwa wakimsubiri Bwana Harusi. Biblia inatuambia watano kati yao walikuwa na busara na watano walikuwa wapumbavu. Busara ya wale watano wa kwanza ni kuwa na taa zenye mafuta ya akiba huku wakimsubiri Bwana, na upumbavu wa wale watano wengine ni kuwa na taa zisizo na mafuta ya akiba huku wakimngoja Bwana harusi pia.
Kwa sababu ya Bwana harusi kuchelewa wanawali hawa wote waliamua kulala. Ule mstari wa sita na saba inasema ‘Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, Bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao’.
Katika sehemu ya pili ya somo hili niliandika kwamba jifunze kuitazama taarifa ya mlinzi kama fursa ya matengenezo. Biblia iko wazi kwamba wanawali hawa waliamua kulala baada ya kuona Bwana harusi wao amechelewa. Kumbuka kwamba lengo la wote hawa ilikuwa ni kumlaki Bwana Harusi. Sasa kilichowaamsha toka usingizini ni ‘kelele za taarifa’ ambazo ninaamini zilikuwa za walinzi ambao jukumu lao ilikuwa ni kutoa taarifa juu ya uwepo au ujio wa Bwana harusi husika.
Kutokana na mfano huu tunajifunza kwamba mosi taarifa ya mlinzi/walinzi iliwasaidia wanawali kuamka kutoka usingizini maana walikuwa wamelala. Licha ya taarifa kuwasiaida kuamka usingizini, taarifa ya mlinzi ilitoa fursa ya wanawali kujiandaa. Tumeona katika mstari wa saba kwamba punde baada ya taarifa wale wanawali wakaamka na kuziandaa/zitengeneza taa zao. Naam taarifa ya walinzi ilitoa fursa ya matengenezo. Hivyo hata sasa Mungu anapoleta taarifa kwako, ujue analeta taarifa ya matengenezo, naam mbele kuna jambo linakuja, hivyo analeta taarifa mapema kupitia walinzi wako au wa eneo lako ili uitumie kutenda yapasayo. 
Jambo la pili – Umuhimu wa kuwa na mahusiano mazuri kati ya Mlinzi na watu wa eneo lake.
Kupitia mfano huu wa wanawali kumi tunagundua pia kwamba, taarifa ya mlinzi ilitoa fursa ya mawasiliano baina yao. Kabla ya taarifa hatuoni wanawali hawa wakiwasiliana kwa jambo lolote. Si hivyo bali pia tunagundua kwamba baada ya taarifa ya mlinzi ndipo fahamu za wale wanawali wapumbavu zikafunguka na wakajua mafuta yao hayatoshelezi. Kwa mujibu wa Biblia harusini aliruhusiwa kuingia mtu (mwanamwali) mwenye taa inayowaka yaani taa yenye mafuta.
Je, ni kwa nini wale wanawali wapumbavu kabla hawajaenda kulala hawakufikiri kwamba mafuta haya yakiisha na hatuna ya akiba hatuwezi kuingia harusini?  Huenda hawakujua kwamba mwanamwali mwenye taa inayowaka ndiye atakayeruhusiwa kuingia harusini. Jambo ninalotaka ulione ni kwamba pamoja na kutokujua kwao, walinzi wa mji walijua nini kinatakiwa kwa mtu kuingia harusini. Laiti wanawali wangekuwa na mahusiano mazuri na walinzi wa mji wangepewa siri kuhusu ujio wa Bwana harusi wao. Lakini kwa sababu hawakuwa na mahusiano mazuri na walinzi, walishindwa kuwauliza wale walinzi mahitaji ya msingi atakapokuaja Bwana harusi. Naam wakajikuta wameachwa na Bwana wao walipoenda kutafuta mafuta. 
Ukweli huu kuhusu mahusiano unathibitishwa katika kitabu cha Wimbo Ulio Bora 3:3 unaosema ‘Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu’. Habari hii inatueleza habari za kijana aliyekuwa anamtafuta mwenza (mpenzi) wake kwa muda mrefu bila mafanikio. Katika kuendelea kumtafuta ndipo akakutana na walinzi wa mji, akawauliza mmemwona mpendwa wa nafsi yangu?          Ni imani yangu walinzi wale walimjibu, kwa sababu mstari wa nne unatumabia ‘kitambo kidogo tu nikishakuwaondokea, nikamwona mpendwa wa nafsi yangu, Nikamshika nisimwache tena…’ Hivyo ufumbuzi wa tatizo (hitaji) la huyu kijana ulipatikana kwa walinzi wa mji. Kwa hakika mahusiano mazuri ya Walinzi na yule kijana yalipelekea hitaji la kijana kufanikiwa au kufikiwa.
Kutokana na habari hii ni dhahiri kwamba walinzi wamewekwa kwenye nafasi zao ili kuleta ufumbuzi juu ya changamoto zinazomkabili mwanadamu kwa kumjulisha mawazo ya Mungu juu yake, ili pia kumsaidia mwanandamu aishi kwa kulitumikia shauri la Mungu katika siku zake. Biblia katika kitabu cha Isaya 62:6-7 inasema  ‘Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Eee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani’.
Mungu anataka yawepo mawasiliano na mahusiano mazuri kati ya Mlinzi (Walinzi) na wanaolindwa. Katika andiko hilo hapo juu, licha ya Mungu kuweka walinzi juu ya kuta za Yerusalemu ilibidi awape taarifa na wakazi wa mji huo, ili wasije, walinzi hao wakatoa taarifa ya kile Mungu amesema na wakazi wa Yesrusalemu wakapuuza, mwisho wao wakaangamia.
Ukisoma pia Biblia katika kitabu cha Mathayo 24:43 inasema ‘Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angalijua ile zamu mwivi atakayokuja, anagalikesha, wala asingeliacha nyumba yake kuvunjwa’. Naam kiroho milinzi au walinzi ndio waliopewa uwezo wa kuona nini kinakuja juu yako, ndoa yako, kazi yako, huduma yako, taifa lako nk. Kwa sababu hii ni muhimu sana kuwa na mahusiano mazuri na mlinzi au walinzi ambao Bwana Mungu amekuweka chini ya Mlango au Himaya yao. Naam kufanikiwa kwa kazi ya mlinzi katika nafasi yake kunategemea mahusiano na ushirikiano anaopata kutoka kwa watu wa eneo lake.   
Mungu akubariki kwa kufuatilia mfululizo huu, usiache kuombea muendelezo wa somo hili. Tutaendelea na sehemu ya nne…

No comments:

Post a Comment