Saturday, April 21, 2012

NINI MATARAJIO YA MUNGU KWA VIJANA?

                                      NINI MATARAJIO YA MUNGU KWA VIJANA?
A
Na: Patrick Samson Sanga.
 1yohana 2:14 “…. Nimewaandikia ninyi,vijana kwa sababu mna nguvu,na neno la Mungu linakaa ndani yenu ,nanyi mmeshinda yule mwovu.”Mungu anao mtazamo wake binafsi juu ya kila kundi la watu chini ya jua,.Na kila kundi mfano wa wamama,wajane,watoto,vijana kuna mambo fulani ambayo Mungu anatarajia kila kundi litatekekleza. Mungu anazungumza na vijana na kusema nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu moja mna nguvu,mbili neno la Mungu linakaa ndani yenu, na tatu mmemshinda yule mwovu.
Nguvu zinazozungumziwa hapa ni nguvu,uweza wa Mungu wa kukusaidia kutekeleza maagizo yake. Na kwa sababu hiyo basi kuna matarajio ya Mungu kwa hao vijana. Sasa lengo la ujumbe huu mfupi ni kukueleza nini Mungu anatarajia/anategemea kwamba utafanya sawasawa na nafasi aliyokupa mbele zake na uwezo aliokupa. Matarajio ya Mungu kwa vijana ni kama ifuatavyo:
*Moja, Vijana wauteke ufalme wake.
Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu,nao wenye nguvu wauteka”. Biblia inapozungumzia ufalme wa Mungu inazungumzia habari za utawala wa Mungu . Hivyo ni matarajio ya Mungu kwamba popote pale vijana walipo basi watatengeneza mzazingira ya Mungu kutawala katika maeneno waliyopo iwe darasani, Chuoni, Kazini, Kanisani nk na hii ni kwa sababu wana nguvu.Sikiliza vijana wana nguvu na ufalme unapatikana kwa nguvu,maana yake Mungu anatarajia vijana watumie nguvu zao kuuteka ufalme wake na kuurusu uchukue utawala duniani.
*Mbili,Vijana warejeshe urithi na mali za wana wa Mungu zilizotekwa.
Mwanzo 14:13-16. “…Akawapa silaha vijana wake,walozaliwa katika nyumba yake,watu mia tatu na kumi na nane,akawafuata mpaka Dani”. Hizi ni habari za Ibrahamu aliyeenda kumuokoa nduguye Lutu baada ya kuwa ametekwa.Ili kurejesha urithi wao na mali zao ilimbidi Ibrahimu atumie nguvu kazi ya vijana. Na hivyo hata leo Mungu anatarajia kwamba vijana wasimame kwenye nafasi zao na kupambana kwa ajili ya afya,ulinzi, uchumi,uponyaji,mafanikio ya watu wake. Hebu jipe dakika moja halafu tazama jinsi shetani anavyotesa watu na kudhulumu afya zao, ujana wao, ndoa zao ,uchumi wao nk.Ni nani watakaorejesha hali nzuri, urithi huu kwa wana wa Mungu , ni Mungu kupitia Vijana.
*Tatu, Vijana wasikosee katika kufanya maamuzi ya kuoa au kuolewa.
Mithali 5:18 “Chemichemi yako ibarikiwe;nawe umfurahie mke wa ujana wako”.Sikiliza Mungu anataka ndoa yako iwe ni ndoa ya mafanikio na ya furaha, maana yake ni ndoa ambayo hautaijutia kwamba kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu mtu.Sasa ili ndoa yako iwe ni ya furaha na amani, ni lazima huyo mwenzi wako umpate kwa uongozi wa Mungu mwenyewe. Sasa mtazamo wa Mungu kwa vijana ni huu vijana hawatakosea kufanya haya maamuzi kwa sababu tayari Neno la Kristo limejaa kwa wingi ndani yao.Kumbuka neno la Kristo ni taa ya miguu yangu.
*Nne, vijana wawe wasuluhishi wa matatizo katika jamii na taifa.
 Mithali 1:4 “Kuwapa wajinga werevu,na kijana maarifa na hadhari”. Leo ndani ya kanisa, jamii tunayoishi na katika taifa kwa ujumla yapo matatizo mbalimbali ya kiroho,kiuchumi,kijamii,kiafya,kimwili,kibiashara,kindoa nk. Sasa Mungu anatarajia vijana ndio watumike kusuluhisha matatizo haya mbalimbali katika jamii kwa sababu ya wingi wa neno la Kristo ndani yao. Hii ina maana mtu mwenye neno la Kristo kwa wingi ndani yake basi maana yake ana upeo mkubwa wa kuelewa mipango na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye matatizo yanayowakabili. Hivyo tumia fursa hiyo kutatua matatizo hayo na kusuluhisha kwa sababu ya Kujua mawazo na njia za Mungu za kuwatoa watu wake kwenye shida walizonazo.
*Tano, vijana walitumikie kusudi lake la kuhubiri habari njema.
 Mathayo 28:19 “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi,mkiwabatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu”. Sikiliza kwa sababu ya nguvu ambayo Mungu amewekeza kwa vijana basi ni matarajio yake kwamba wewe kama kijana utatumika kuwaeleza watu wengine habari njema za Yesu Kristo ziletazo amani. Ni matarajio yake kwamba vijana watapita nyumba kwa nyumba , mtaa hadi mtaa wawaambie wengine kuhusu huyu Yesu, wakiwafungua waliofungwa na kuutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika. Naamini haya matarajio matano ya Mungu kwako kama kijana mwenzangu basi yatakusaidi sasa kukaa kwenye nafasi yako ili Mungu ajivunie kuwa na kijana kma wewe.
Amani ya Kristo na iwe pamoja nanyi.

4 comments:

  1. Hongera sana dada kwa mafundisho mazuri. Mungu akubariki.
    Nashauri pia uangalie namna ya kubadilisha Background na rangi ya maneno hayo ili kuleta uepesi katika kusoma.

    kazi yako ni njema na Mungu atakulipa.

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  3. Amina! Ujumbe nzuri kwa vijana
    Barikiwa!

    ReplyDelete
  4. Amen!ujumbe nzuri sana kwa vijana

    ReplyDelete