Friday, April 20, 2012

MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO



MWANAMKE, SIMAMA KWENYE NAFASI YAKO ILI UWEZE KUIPONYA NDOA YAKO

Na: Patrick Sanga
Namshukuru Mungu ambaye anazidi kunipa neema ya kuandika na kuandika masomo mbalimbali na pia yale yanayohusu akina mama hasa wao kuwa kwenye nafasi zao.
Mnamo Novemba, 2009 mama mmoja alinitumia email akinieleza kwa jinsi ambavyo ndoa yake imekuwa ikimsumbua na kufika mahali pa yeye kujutia hata kwa nini alikubali kuolewa. Baada ya kupata ujumbe wake nilichukua hatua ya kufanya maombi kwa ajili ya huyu mama na wengine wenye shida kama yake kwenye ndoa zao. Katika kuomba, Mungu alinisemesha na kunifundisha kupitia Biblia mambo ya msingi ambayo sasa nimeona ni vema nikayaandaa kama somo na kuweka kwenye blog ili kila nafsi ya mwanamke yenye kuhitaji haya maarifa iweze kuyapata, maana imeandikwa katika Mithali 19:2 kwamba ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa’.
Mambo manne yafuatayo kama ukiyaweka kwenye matendo nina uhakika yataleta mabadiliko/uponyaji na pia kujenga msingi imara wa ndoa yako. Mambo hayo ni kama ifuatavyo;
  • Sharti wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao.
Hili lilikuwa jambo la kwanza Bwana kunijulisha, ili niwakumbushe tena akina mama. Nimeshaandika kuhusu nafasi za Mwanamke huko nyuma, kwa ufafanuzi zaidi bonyeza link hii http://sanga.wordpress.com/2006/10/23/wanawake/. Kwa kifupi niseme uponyaji wa wa ndoa yako upo kwa wewe kuwa kwenye nafasi yako. Mungu hana namna ya kukusaidia kama hauko kwenye nafasi yako.
Ni lazima uzijue nafasi ambazo Mungu amekupa na kisha kusimama vema ukiwajibika kwenye hizo nafasi. Kinamama wengi leo wanalia sana Mungu aponye ndoa zao na matokeo yake yanakuwa tofauti na matarajio yao. Endapo kama na ndoa yako ipo kwenye eneo kama hili, angalia kama umekaa vizuri kwenye nafsi ambazo Mungu amkupa katika ulimwengu wa roho. Nina uhakika unaweza ukawa kuna maeneo ulijisahau hivyo tengeneza, maana uponyaji na uharibifu wa ndoa yako kimaandiko upo katika uwezo wako mama.
Ni maombi yangu kwamba Roho Mtakatifu akujulishe jambo hili, uponyaji wa ndoa yako haupo kwa Mungu, bali Mungu ameweka uwezo huo ndani yako. Ili uwezo huo uweze kufanya kazi sawasawa ni jukumu lako kuwa kwenye nafasi zako.  
  • Unahitaji hekima ya Mungu ili kujenga ndoa yako
Ukisoma kitabu cha Mithali 14:1 Biblia inasema “Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe”. Biblia imeshaweka wazi kwamba wewe unaweza kuijenga au kuibomoa nyumba yako. Uwezo wa kufanya jambo hili unategemea kiwango cha hekima ya Mungu ambayo ipo ndani yako na juu yako pia. Hekima ya kuponya ndoa yako ambayo sasa unajua iko mashakani, ipo kwenye neno la Mungu na si kwa waganga wa kienyeji.
Unaipataje hekima ya Mungu?
Katika Mithali 8:1 Biblia inasema ‘Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake?’ mstari wa 10 unasema ‘Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi’. Ule mstari wa 14 unasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu, mimi ni nguvu’. Na ule wa 16 unasema ‘Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’.
Siku zote kama unataka hekima ya Mungu ya kukusaidia kwenye eneo lolote la maisha yako utaipata kwenye neno la Mungu au kwa Mungu.  Imeandikwa katika Mithali 12:1a “Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa’. Hekima ya Mungu kwa mtu ni matokeo ya kiwango cha neno la Mungu ambalo mtu ameliweka na kulitafakari kwa wingi moyoni mwake. Kwa hiyo kwa Watawala, hekima ya Mungu kwa Mtawala inategemea kiwango cha neno la Mungu kuhusu utawala ambalo Mtawala amekiweka ndani yake. Naam hekima ya Mungu kwa Mwanamke itategema kiwango cha neno la Mungu kuhusu nafasi zako ambacho umekiweka ndani yao nk.
Sharti neno la Mungu kuhusu nafasi zako, wajibu wako nk liwe kwa wingi ndani yako ndipo hekima ya Mungu ya  kujenga nyumba/ndoa/familia yako itakapokaa ndani yako na juu yako. Na kwa kuwa hekima ni ufahamu, maarifa, shauri na nguvu, itakusaidia katika kuijenga ndoa yako, kama inavyowasaidia watawala, waung’wana na waamuzi katika majukumu yao (Mithali 8:16). Naam hekima hiyo itaongoza kinywa chako kuleta uponyaji wa ndoa na nyumba yako, kama Biblia inavyosema katika Mithali 31:26 “Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake”.
Mithali 8:17 inasema ‘nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’. Naam siku zote, hekima inawasiaidia wale wanaoitafuta na wakaipata’. Na njia kubwa ya kupata hekima hiyo ni kwa njia ya kusoma na kuatafakari neno la Mungu kila siku na kuomba kama nilivyokufundisha hapo juu.
  • Uwe makini kufuatilia maisha ya mume wako/watu wa nyumbani mwako
Mithali 31: 27 “Huangalaia sana njia za watu wa nyumbani mwake; wala hali chakula cha uvivu”. Tafsiri ya kiingereza ya BBE inasemaShe gives attention to the ways of her family; she does not take her food without working for it”. Moja ya nafasi za mwanamke ambayo nilishaandika huko nyuma ni kuwa mlinzi wa mwanaume, hii ikiwa ni pamoja na mume wake.
Naam jukumu la ulinzi ni kubwa sana ambalo Mwanamke umepewa, siku zote mlinzi ana wajibu wa kufuatilia kwa karibu sana maisha/nyendo za yule  anayemlinda. Kwa dhana ya ndoa yako, ni jukumu lako kama mlinzi kufuatilia maisha ya mume wako na kujua kama anaishi katika mapenzi ya Mungu. Naam ukijua anaishi nje ya mapenzi ya Mungu simama kwenye nafasi zako uendelee kuomba huku ukiamini Mungu atambadilisha na kumsaidia kuishi katika mapenzi yake.
Kuwa makini kufuatilia maisha na njia za mume wako, itakusaidia kujua hali yake, na hatari ambayo inataka kumpata, hivyo kama mumeo ameokoka au ni mcha Mungu utakuwa na jukumu la kumtahadharisha kwamba awe makini na baadhi ya vitu ambavyo umeona asipokuwa makini navyo ataanguka. Naam kama hajaokoka na ni mtu ambaye hamjui wala kumjali Mungu, usikate tamaa na isikufanye ukaondoka kwenye nafasi yako, dumu hapo ukijua kwamba Mungu ni mwaminifu atafanya kwa kuzingtia maagizo yako kama mlinzi.
  • Usisubiri hadi tatizo litokee ndipo uanze kutafuta msaada wa Mungu
 Jifunze kutumia wakati wa amani kuweka msingi mzuri wa ulinzi kwenye ndoa yako. Usisubiri wakati wa hatari ndipo ujipange kwa mapambano. Ki Mungu kila siku kwako ni siku ya kujenga au kuongeza ukuta wa ulinzi kwa nyumba yako.   Sehemu kubwa ya maombi ambayo akina mama wanapeleka kwa Mungu ni ili apate kuziponya ndoa zao kwa sababu zimeingia kwenye matatizo. Sijui kama unaona jambo hili, wengi wanaomba kwa sababu ndoa zao zipo kwenye shida. Naam Mungu anataka ujifunze kuomba ulinzi wa ndoa yako wakati ndoa yako ina amani, tumia vizuri wakati wa amani kujenga kuta za ulinzi kwa ndoa na nyumba yako kwa ujumla.
 Ni imani yangu kwamba ujumbe huu, umekuongezea kwa kiasi fulani maarifa ya kukusaidia katika kuijenga ndoa yako. Jambo la msingi kujua ni kwamba, Katika kubadilisha maisha ya mume wako na kuiponya ndoa yako, Mungu anaangalia kwanza kama umesiamama kwenye nafasi zako na unatekeleza wajibu wako.
 Neema ya Kristo iwe nawe

3 comments: