JIFUNZE KUFIKIRI KABLA HUJACHUKUA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Na: Patrick Samson Sanga
Nawasalimu kwa jina la Yesu . Leo katika nyanja hii ya vijana, nimeona ni vema tukashirikishana kuhusu suala la ‘kufikiri kabla ya kuoa au kuolewa’.
Siku moja katika kusoma Biblia nilikutana na mstari ufuatao, nakusahuri uusome kwa umakini. Biblia katika 1Wakorinto 7:8-9 inasema “Lakini
nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi
nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa
kuliko kuwaka tamaa”.
Baada ya kuusoma mstari huu niliingia katika tafakuri nzito sana
ambayo mwishowe ilinipeleka kuandaa somo hili, kwamba ni vema ukafikiri
vizuri kabla ya kuchuka uamuzi wa kuoa au kuolewa.
Unajua malezi, dini, madhehebu yetu, wazazi, mila na desturi
vinachangia kwa kiwango kikubwa sana kuhusu utaratibu wa kuanzia mtu
kupata mke au mume mpaka watakapofunga ndoa. Kila kundi lina mfumo na
utaratibu wake ambao lingependa vijana waufuate ili kuhakikisha wanaoa
na kuolewa kwa kile ambacho kila kundi linaona na kuamini kwamba huo
ndio uataratibu mzuri kufuatwa.
Namshukuru Mungu kwa kuwa nami nimeoa, ingawa vitu vingi sana Bwana
alikuwa ananifundisha vinavyohusu ndoa hata kabla sijaoa. Nakubaliana na
dhana kwamba ili uweze kuwa Mwalimu mzuri kwenye nyanja fulani basi ni
lazima au ni vema wewe mwenyewe ukawa umepitia kwanza kwenye nyanja
hiyo. Lengo ikiwa sio tu ufundishe ‘theory’ bali pia utufundishe na
uzoefu wako binafsi kwenye eneo hilo. Licha ya kukubaliana na dhana hii,
kwangu binafsi haikuwa hivyo, maana kuna mambo mengi ambayo, Bwana
Yesu, alikuwa ananifundisha yanayohusu ndoa hata kabla sijaoa.
Kwa kifupi ndoa ni shule au darasa ambalo wanandoa wanatakiwa kukaa
chini na kujifunza kila siku namna ya kuishi humo ndani ili kuweza
kuishi maisha ambayo Mungu amewakusudia.
Kutokana na mifumo ya baadhi ya makanisa yetu, si vijana wengi ambao
wanafundishwa kwa undani kuhusu maamuzi haya makubwa. Wengi wao
wameingia kimwili na kujikuta wakijutia na kulaumu kwa nini nilimuoa au
kuolewa na huyu kijana. Nasema haya kwa kuwa nimekutana na
wanandoa wengi wa aina hii, na nataka nikuambie kama Biblia ingetoa
mwanya wa wanandoa kuachana na kuoa au kuolewa na mtu mwingine, wapendwa
wengi sana walioko kwenye ndoa wangefanya hivyo na wengine
wasingekubali kuolewa au kuoa tena.
Unajua kwa nini?
Ni kwa sababu si vijana wengi wenye ufahamu wa kutosha juu ya aina ya
maamuzi wanayotaka kuyachukua. Kwa hiyo katika somo hili nimeona vema
niandike mambo manne ya msingi ambayo naamini yataongeza na kupanua
ufahamu wako ili kukusaidia kufikiri kwanza kabla ya kufanya maamuzi
haya makubwa;
- Si kila ndoa inayofungwa imeunganishwa na Mungu, kwa kuwa ndoa ni kiungo cha muhimu kwa Mungu na Shetani pia.
Kuanzia mwaka 2005, Mungu alinipa kibali cha kuanza kufundisha na pia
kushauri juu ya mambo kadhaa kuhusu wanandoa. Tangu wakati huo hadi
sasa nimekutana na baadhi ya wanandoa ambao wanajuta kwa nini walikubali
kuoa au kuolewa. Wanaishi kwenye ndoa kwa sababu tu ya watoto na pia
kwa hofu kwamba endapo kama wataachana jamii na watu wanaowazunguka
hawatawaelewa.
Ni vizuri ukafahamu kwamba si kila ndoa inayofungwa ni ya mapenzi ya
Mungu, hata kama imefungwa kanisani. Biblia inaposema kilichounganishwa
na Mungu, mwanadamu asikitenganishe, katika nafasi ya kwanza maana yake
iwe ndoa ambayo Mungu ndiyo aliyehusika katika kuanzisha mahusiano na
kuwaongoza hao watu kuishi pamoja. Wakati Mungu anatafuta kuhakikisha
watu wake wanaoana katika mapenzi yake na Shetani naye anapambana
kuhakikisha watu wanaoana katika hila (mapenzi) zake.
Shetani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kuvuruga wanandoa wengi
na kuwafanya waishi maisha tofauti na yale ambayo Mungu aliwakusudia. Ni
kwa sababu hii ndio maana Paulo aliwaambia Wakorinto ‘Lakini nawaambia
wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo,
lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko
kuwaka tamaa’. Paulo aliona shida, maudhi ya wandugu walioko kwenye ndoa
tokana na migogoro aliyokuwa akikutana nayo.
Fahamu kwamba ni furaha kubwa kwenye ufalme wa giza mtu
anapooa au kuolewa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu
Shetani anajua akifanikiwa kukushawishi ukaoa kinyume na mapenzi ya
Mungu, ameharibu ‘future’ yako na kile ambacho Mungu alikusudia ukifanye
hapa duniani. Kumbuka suala sio kuoa au kuolewa tu, bali ni kuingia
kwenye ndoa ambayo itakuwezesha kulitumika shauri la Bwana katika kizazi
chako. Hivyo kabla hujaamua nani uishi naye hakikisha unamshirikisha
Mungu akuongoze kumpata mwenzi sahihi.
- Unapaswa kuoa au kulewa katika mapenzi ya Mungu
Naam kuoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu ni changamoto nyingine
kubwa kwa vijana wa kizazi cha leo. Naam hili ni eneo ambalo Mungu yupo
makini sana kufuatilia nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Na upande wa
pili nao, Shetani anapigana kwa juhudi kubwa ili kuvuruga kusudi la
Mungu kupitia mtu au watu.
Ni vizuri ukafahamu kwamba unapotaka kufanya maamuzi ya
kutaka kuoa au kuolewa, Shetani naye ataleta mawazo (mapenzi) yake ndani
yako juu ya nani anafaa zaidi kuwa mwenzi wako maisha. Lengo
lake ni kuhakikisha anakuunganisha na mtu ambaye anajua kwa huyo
atakumaliza kiroho na kihuduma kabisa. Suala sio kuwazuia msiende
kanisani, bali ni kuhakikisha kile ambacho ungefanya kwa kuwa na mtu
sahihi hakifanikiwi. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hili, muulize
Mchungaji wako, kesi nyingi anazokutana nazo kanisani kwake zinahusu
nini, naamini atakujibu kimapana. Ni jukumu lako kuwa makini kufuatilia
unatii wazo la nani, Mungu au Shetani?
- Vigezo vya kimwili ni silaha kubwa ya uharibifu
Vigezo vya kimwili ni moja ya silaha kubwa ambazo Shetani anazitumia
kuwavuruga watu wengi waweze kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu
kwao. Jifunze kufukiri na kutafsiri mambo au makusudi kama Mungu
anavyotazama na kutafsiri. Na uwezo wa kufanya hili utaupata kwenye neno
lake tu. Kwako mwanaume Mungu anapokupa mke anakupa Mlinzi na msaidizi.
Na kwa mwanamke Mungu anakuwa amekupa kichwa. Ni muhimu sana kuchunga
ni msaidizi, mlinzi au kichwa gani unataka kiunganishwe na maisha yako
kwa njia ya ndoa.
- Ndoa ni wajibu mkubwa
Ndani ya ndoa kuna wajibu mkubwa sana unaokusubiri kama baba au mama.
Ndani ya ndoa muda na uhuru wako unabanwa na mwenzi wako. Ndoa inabana
pia muda wa kuwa na Mungu wako. Na kwa wengi kwa kutaka kuwapendeza
zaidi waume au wake zao, wamefarakana na Mungu, kwa sababu wamewapa
waume au wake zao hata nafasi na muda wa Mungu kwenye maisha yao.
Usiingie ndani ya ndoa kwa fikra za uapnde mmoja. Naam ndoa ni wito
wa mapungufu na uvumilivu ambao ni lazima uwe tayari kuchukuliana na
mwenzi wako katika mapungufu yake. Kuna vitu hamtaweza kufanana na kwa
sababu ya mapungufu yaliyopo kwa kila mmoja unapaswa kutafakari kuhusu
majukumu yanayokuja kwako kama mwanandoa, hekima na busara katika
kuzikabili changamoto za ndoa, kama vile kuzaa au kutokuzaa,
kutokujiweza katika masuala ya unyumba, matumizi ya fedha, tabia za
mwenzi wako nk.
Haya ni mambo ya kuhakikisha unayaombea mapema ili kujenga msingi
imara utakapoingia kwenye ndoa yako. Lakini nikutie moyo kwamba endapo
utaoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu, yeye ni mwaminifu,
atakuunganisha na mtu ambaye katika changamoto mtakazokutana nazo
hazitawakwamisha wala kuwafanya mjute. Bali endapo Shetani ndiye
ataongoza maamuzi yako, ni majuto makubwa sana (asomaye na afahamu).
Mungu akubariki, naamini ujumbe huu umeongezea mambo ya kutafakari na kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi wa kuoa au kuolewa.
No comments:
Post a Comment