Friday, April 20, 2012

JINSI YA KUUJENGA NA KUUKUZA UJASIRI WAKO (Boosting your self Confidence)

by samsasali.blogspot.com

jitambue Ya Chris Mauki....JINSI YA KUUJENGA NA KUUKUZA UJASIRI WAKO (Boosting your self Confidence)


Katika kufanikiwa katika jambo lolote unahitaji walau mambo yafuatayo;
  1. Unahitaji kujua kile unachokitaka
  2. Unahitaji shauku ya hali ya juu ya kupata kile unachokihitaji.
  3. Unahitaji kuamini kwamba unaweza kukipata kile unachokihitaji, yaani kuuamini uwezo ulionao katika kuhakikisha unakipata unachokihitaji.
  4. Unahitaji kuamini kuwa unastahili kukipata unachokihitaji. Namanisha kujiamini kuwa unathamani kabisa kukimiliki unachokitaka.

Ujasiri ninaokwenda kuuzungumzia hapa unahusika moja kwa moja na jambo la tatu na la nne.

Tuanze na jambo la tatu: Amini kwamba unaweza kukipata au kuwa nacho kile unachokihitaji.
Kuamini kabisa ndani yetu kuwa tunauwezo wa kukipata au kuwanacho kile tunachokihitaji ni sehemu ya kwanza na muhimu katika kupata ujasiri. Habari njema ni kwamba kila mmoja anauwezo. Tunachokihitaji tu katika kuamini hili ni kujikumbusha sisi wenyewe baadhi ya vitu muhimu.

1. Wakati wowote wazia mafanikio
Najua yako mafanikio mengi umeshawahi kuyapata kuanzia  utoto wako. Yamkini mengine yawezekana kuonekana kituko lakini ukiyawaza sana na kulinganisha na muda ule, utajua kweli kuwa yalikuwa ni mafanikio makumbwa. Mfano vitu kama kujifunza na kufanikiwa kutembea, kufanikiwa kuzungumza, hata kwa lugha ya kwenu. Kama wewe uliweza, wakati kuna waliopata shida sana ili kuweza  basi bado unaweza kufanya mwakubwa zaidi.

2. Zipo nyakati utahitaji msaada wa wengine
Katika yale yote unayodhani utayahitaji ili ufanikiwe, usisahau kuwa utahitaji pia msaada wa mtu au watu wengine. Na hapa utafahamu kuwa hakuna hata mmoja anayeweza kufanikiwa kwa kujitememea mwenyewe. Hata ukijiangalia wewe kama unajiona uliyefanikiwa, utajua wazi kuwa kuna wengine ambao walikuwezesha kuwa hapo ulipo kwa namna moja au nyingine. Kwa kulitambua hili utaamini kuwa kwa mafamikio yote ya mbeleni, wapo wengine watakaolazimika kutubeba, kutushika mkono na kutusaidia tufike kule tunakotaka kufika.

3. Fahamu kwamba umeumbwa na uwezo wa ajabu
Uwezo tulioumbwa nao waweza kutumiwa vyovyote vile pale uhitaji unapokuwepo. Hii inamaanisha kwamba hata katika nyakati ambazo tunashindwa bado tuna uwezo wa kujifunza ni kwanini tumeshindwa na kwa hivyo tunaendelea mbele vema zaidi.

Ili kujiamini wewe mwenyewe yakupasa pia ufahamu kwamba utendaji wako wa sasa na utendaji wako wowote wa nyakati zijazo sio alama au kielelezo cha kuonyesha uwezo ulionao. Utendaji wako ni kionyesho tu cha ulivyofanya au ulivyotenda kwa wakati fulani, ukiwa katika hali Fulani na sio kwamba ndio tabia au uwezo wako. Uwezo wako kamwe hauwezi kulinganishwa na utendaji wako, ndani yetu tuna uwezo mkubwa zaidi ya tunavyofikiri na uwezo huu ni zaidi ya vile tuvitendavyo au kuvifanya kila siku.

4. Uwezo ulionao una mipaka au ukomo
Ingawa uwezo tulionao ni mkubwa lakini pia una mipaka au ukomo. Nguvu au uwezo wa Mungu pekee ndiyo usio na mipaka na ukomo. Katika hili itakuwezesha kuamini kuwa ingawa ziko nyakati unajiona huwezi au hutoweza, Mungu anaweza kukuwezesha hata katika yale ambayo nguvu au uwezo wa mwanadamu unafikia ukomo na utaweza kusema  kuwa “hapa nisingeweza kwa nguvu zangu mwenyewe“

Ø  Kuza ujasiri wako kupitia ukiri wenye kujenga (Positive affirmation)
Tumeona kwamba sisi wote tuna nguvu au uwezo wa ajabu na uwezo huu hauonyeshwi tu kupitia utendaji wetu. Kwa kulijua hili na kwa kuyawezesha mawazo yako kila siku katika kulijua na kuliamini hili inakubidi ujifunze kuyazoeza mawazo yako kuongea au kukiri vilivyo vya kujenga.
-          kwa kukiri huku unaujenga mwili na akili yako kuamini kuwa unaweza.
-          Maneno haya ya ukiri wenye kujenga na kutia moyo yako mengi, yaweze kuwa ni maneno yaliyosemwa na watu mashuhuri, au wahenga (nahau), yaweza kuwa maneno kutoka vitabu vitakatifu au nyimbo Fulani n.k. Nitajaribu kutoa mifano michache hapa.
Maneno yenye fikra chanya (Words with positive thinking)
-          kama wao waweweza, mimi nishindwe kwa nini?
-          Kama hakuna aliyewahi kuweza, basi nitakuwa wa kwanza kuweza au kufanya.
-          Uko uwezo ndani yangu ambao bado sijawahi kuutumia.
-          Hata kama sijafanikiwa sasa, nitajaribu tena na tena hadi nione tofauti.
-          Nitajitahidi kupata upenyo katika lolote bila kujali hali itakavyokuwa.
-          Ingawa wamesema na wanaendelea kusema kwamba sintashinda, nitajitahidi kuhakikisha wanauona ushindi wangu.
-          Nayaangalia mambo ya maisha kama changamoto sio kama matatizo
Dondoo zilizowahi kusemwa na watu mashuhuri (Quotes)
-          Mwanadamu hakuwahi kuumbwa ili  kushindwa – Ernest Hemingway
-          Ni furaha na jambo jema sana kufanya vilivyo shindikana – Walt Disney.
-          Kamwe haujachelewa kuwa vile ulivyowahi kutamani kuwa (George Elliot)
-          Mwanadamu haitwi mzee mpaka pale majuto yanapochukua nafasi ya ndoto zake – John Barrymore,
-          Kati ya miujiza na ugunduzi wa kushangaza kuliko yote ni pale mwanadamu anapoweza kufanya lile alilokuwa akihofia kushindwa kulifanya  (Henry Ford).

Amini kwamba unastahili kuwa na kile unachotamani kuwa nacho
Kuamini kwamba unastahili kuwa na kitu ni alama ya ujasiri binafsi ambayo inahusianishwa na kuitambua thamani uliyonayo. Kama unafikiri kuwa wewe sio mtu mwenye thamani basi kamwe hutajiona unastahili vitu vizuri katika maisha na pia kutowahi kuvipata viyu hivyo. Kwa hiyo anza kuviendea hivyo unavyohisi unastahili au la sivyo kaa ukivifurahia vile vilivyo katika uwezo wako tu
-          Fahamu kuwa wewe ni mtu wa thamani isiyopimika, umeumbwa kwa jinsi ya ajabu.
-          Cha muhimu sana kuzingatia na kujua ni kwamba hakuna kosa lolote la kimaumbile, kisaikolojia, kibaiolojia au kihisia litakaloweza kuishusha thamani yako.
-          Uthamani wetu hauwezi kamwe kuathiriwa na vile tunavyoweza au tusivyoweza kuvifanya.
-          Epuka kuchanganya kati ya uthamani wako na makosa au madhaifu unayoweza kuyafanya, ukiweza hili litasababisha mlipuko wa ujasiri ndani yako.

(a)   Jifunze kujipenda wewe mwenyewe kama hatua ya kuikubali thamani yako
Tunaweza kuwaweka watu katika makundi matatu ya namna wanavyojipenda wenyewe.
-          kundi la kwanza ni wale wanojidharau wenyewe.
-          Kundi la pili ni wale ambao wamejikubali
-          Kundi la tatu ni wale ambao hufurahishwa sana na jinsi walivyo (hujipenda).

Wale wanaojidharau.
Kujidharau huku hutokana na kuchangaya kati ya jinsi tulivyo na nini tuvifanyavyo. Watu wanaojidharau hujisikia vibaya juu yao wenyewe, hasa wanapotambua kuwa wana makosa ya kibinadamu. Wanafikiri kwamba madhaifu waliyonayo yanapunguza uthamani wao.

Wale wanaojikubali
Hawa ni wale ambao huvumilia kutokana na madhaifu fulani waliyonayo ambayo wamehisi hawayapendi na wala hawawezi kubadilisha chochote zaidi ya kuishi na madhaifu yao.
  • Kujikubali sio kujipenda, ndio maana watu wanaojikubali tu hawawezi kuishi katika kiwango cha juu cha kuuthamini uthamani wao. (wanabaki tu kujikubali)
  • Lazima tuweze kwenda mbali zaidi ya kujikubali na kufikia kufurahishwa na jinsi tulivyo.

Wale wanaofurahishwa na jinsi walivyo
Hawa ni wale wanaofahamu na kuujua uthamani wao. Hawa hufahamu dhahiri kuwa hakuna udhaifu wowote katika kuzaliwa au katika makuzi au matendo yao utakaoweza kuathiri uthamani wao. Hawa ni wale ambao huamka kila asubuhi na kuisalimia siku  mpya kwa maneno ya kusisimua kama vile “Hii ndiyo siku njema” “siku njema tena imewadia” sio wale wanaoamka na kusema “Bora jana kuliko leo”.

(b)   Jinsi gani ya kuimarisha uthamani wetu kupitia tabia nzuri katika maisha ya kila siku
-          Hali ya mtu kujiona anathamani au la huboreshwa au kudhoofishwa na yale mambo mtu huyo anayoyafanya katika tabia za kila siku.
-          Nataka nikupe baadhi ya ushauri ili kujiona kwako mwenye thamani kuboreshwe na wala kusidhoofike.



i) Kubali pale unaposifiwa bila kuongeza neno lolote juu yake
Mtu anapokusifia kwa namna yeyote huna sababu ya kuongeza neno lako lolote juu ya sifa ile uliyoipokea, kwamaana kwa kufanya hivyo unaweza kuua maana nzima ya sifa  ile. Mfano; unaambiwa “umependeza sana” unachopaswa kusema ni “Asante” hata kama umependa au hukupenda ulichokivaa jibu ni moja tu “Asante” kama hujapenda labda ni matatizo yako tu.
Utakuta mwingine anaambiwa “umependeza” anajibu “eeh, nilijua leo mtasema nimependeza” au “hata mi najua, mke wangu kaniambia nimependeza”.
Au  unaambiwa “umependeza” unajibu  “ila hii ndiyo nguo pekee inayonitosha” Au “wala siyo yangu hii”  Katika hali hizi unajishushia uthamani wako wewe mwenyewe.

(ii) Kubali pale inapopandishwa cheo bila kuongeza neno lolote
Haikupi thamani yoyote pale unapopewa nafasi kubwa au kupandishwa cheo au kupewa wadhifa wowote na ukaongeza neno la ulinganifu wowote.
Mfano: umepandishwa cheo, na unasema
“Mh. Kweli hawajaona mtu wakumpa hii ofisi, mimi sidhani kama nitaweza”
“Ndiyo wameniona mimi sasa kwa maana wazuri wote wameshahama”
“Mh sidhani kama nitaweza kuongoza kwa kiwango cha wenzangu.
“Hapa lazima niumbuke”
Unachotakiwa kufanya ni kukubali kuwa wakati wako wa kupandishwa cheo umefika na hao waliokupendekeza waliona uwezo wako kwanza.

(iii) Usinunue bidhaa zenye thamani ya chini (feki) wakati bidhaa zenye ubora zina gharma ya kulingana au zina tofauti kidogo sana.
Bidhaa au vitu unavyovitumia kila siku au kuonekana navyo kila mara vinatosha kuonenyesha thamani yako.
Mfano; Gari unayoendesha, nguo unazovaa, viatu vyako, leso unayotumia, soksi, pochi unayobeba, mafuta unayopaka n.k.
Mfano mwingine; unanunua wapi nyama pale unapohitaji kula nyama? Gengeni? wenye vibanda vya utumbo? kwa wanaotembeza? (ambako kote huku usafi na usalama sio wa uhakika) au katika bucha inayotambulika ambako usafi na usalama vinahakikishwa na huduma ni haraka.

Taxi zote katika kituo fulani ni bei moja kwa safari ya umbali wa kufanana, kwanini uingie kwenye taxi iliyoisha ambayo usalama wako uko mashakani, na hata unaposhuka hapo unapoenda watu wanaanza kukushusha thamani yako.

(iv) Usipende kuingiza mwilini mwako vitu vyovyote visivyo vya kiafya na vinavyo haribu mwili wako haraka au taratibu.
-          Ni kutokujithamini pale unapokula chakula kisicho bora kiafya. Labda tu unapokuwa katika hali tete kama vile ukiwa jela.
-          Huhitaji hela nyingi kula chakula bora. Wengi hujitetea kula vyakula vibovu wakisingizia fedha. Si kweli, tatizo watu hawa wanathamini vitu vingine kuliko miili yao.
-          Hatari pia ni pale tunapoweka vitu vya kudhuru na  vyakufisha mwilini mwetu, kama vile madawa ya kulevya, pombe, sigara, madawa ya kujichubua ya kumeza au ya kujipaka, kujitoga hovyo nk. Hii yote inasababishwa na kutojithamini. Anayejithamini hawezi kufanya hivi, hamna aliyewali kufanya haya yote na akasema ametosheka au ameridhika kwa kufanya anachofanya. Fahamu uthamani wako.

(v) Pata muda wa kuvifurahia na kuvikubali vitu vizuri ambavyo umewahi kuvifanya katika maisha.
Katika kuvifurahia na kuvikubali vile tulivyowahi kuvifanya maishani inatupa kuuona uthamani wetu.
Wanasaikolojia  wamegundua kuwa sababu kubwa inayofanya watu wengi kuwa na hofu sana ni kwa kule kujiona au kujihisi wasio na thamani au wenye thamani ndogo. Watu hawa hufikiri kuwa hawana sababu ya kufurahia maisha na wakati wote wanaahirisha furaha hizi wakidhani iko siku moja itakuja na wao watafurahia, na siku hiyo kamwe haijawahi kutokea na wala haitokuja kutokea.
Kama kuwezi kufurahia vile ulivyowahi kuvifanya basi furahi kwa vile vitu ambavyo Mungu alikutumia wewe kuvifanya, hata kama ni vidogo. Shukuru kwa uzima ulionao, nguvu na afya. Katika kila mradi au katika kile unachokifanya (mfano ujenzi wa nyumba), kwa hatua yoyote kilipofika jipongeze. Katika kujipongeza huku unapata nguvu ya kujithamini na kuangalia mbele zaidi.

d) Tujifunze kuwajengea ujasiri wale waliochini yetu
Najua wawezakuwa unajiuliza na kupapasa kujua nini kilikuwa chanzo cha wewe kutokuwa jasiri. Makala hii imekupitisha maeneo mbalimbali kukuwezesha kujikwamua na kujijengea ujasiri ili uweze kuyabadili maisha yako. Lakini naona ni vema tumalizie kwa kujifunza jinsi ya sisi kuwa msaada kwa walioko chini yetu katika kuwajengea ujasiri. Kama nilivyogusia awali, wengi wetu hawana ujasiri leo kwa jinsi mazingira ya makuzi yao yalivyokuwa. Wapo walio wahi kunyanyasika na kunyimwa fursa za kusema kitu mbele ya watu wazima, wako waliokuwa wanapingwa katika chochote kile walichowahi kukiongea. Sio kupingwa tu, nafahamu pia wako waliokuwa wanapokea kipigo baada ya kujaribu kitu na bahati mbaya wakakosea kidogo. Watoto hawa walitendewa haya katika mazingira ya mashuleni au hata manyumbani, hapa namaanisha walifanyiwa haya na walimu au hata wazazi au walezi wao pasipo kujua kuwa walikuwa wanapanda mbegu ya kuua ujasiri katika maisha mazima ya utu uzima wa watoto hao.

Yamkini wewe ni mzazi, kila unaporudi nyumbani unamwona motto wako anabadilika, anaogopa kukaa nawewe au kusema na wewe kitu chochote wakati hana kosa lolote, usinyamaze kimya, labda kuna mazingira anayoishi na kukuzwa akiwa shuleni yanayo muharibu taratibu. Yamkini pia wewe ni mwalimu na unamshangaa mtoto fulani jinsi alivyo muoga, anayejificha nyuma ya wenzake na asiyejaribu chochote, katika hili hutakiwi kunyamaza kimya, labda kuna maisha motto huyu anayaishi na kukuzwa nyumbani ambayo yanaharibu utu na ujasiri wake.

Bahati mbaya athari za makuzi haya hazionekani kwa dhahiri sana mtoto awapo mdogo, bali yeye mwenyewe anapokuwa mkubwa anajishangaa yuko tofauti na wengine.  Lile analolitamani kulifanya au kuliongea anajikuta hawezi kwasababu hana ujasiri hata chembe. Kila ndoto aliyowahi kuwanayo awali inafifia taratibu na mwisho ina kufa. Katika mazingira haya wakulaumiwa ni wazazi, walezi au wanaotoa makuzi mashuleni. Wito wangu kwa sisi wote ambao tunazungukwa na jamii ya watoto ni kwamba tujitahidi sana kuthamini ilembegu ya ujasiri ambayo watoto wanaotuzunguka wamezaliwa nayo. Iwe ni watoto wetu au wawenzetu, sote tunawajibika kukuza na kuendeleza chembe ya ujasiri ambayo watoto hawa wanayo ili waweze kuiona kesho yao yenye mafanikio makubwa. Mimi kama mshauri wa kisaikolojia nimepata nafasi maranyingi sana ya kuzungumza na vijana wakubwa au watu wazima wengi ambao wamekuja kufahamu wakiwa watu wazima kuwa chanzo cha wao kutokuwa na ujasiri ni makuzi waliyopokea kwa wazazi wao. Watu hawa wengi wao wameendeleza chuki kubwa sana na wazazi wao kwavile wamekuwa wakijitazama kama  waliodhulumiwa kitu muhimu sana maishani. Wako walioweza kusamehe ingawa kwamaumivu makubwa sana. Badala ya kuwa wakala wa kuua ujasiri wa walewadogo wanaotuzunguka tuwe mawakala wazuri wa kukuza na kujenga ujasiri wao.

Vifuatavyo vitakusaidia kujenga ujasiri wa watoto wadogo au wengine wote wanaotuzunguka. Kwanza inabidi tujifunze kuwatia moyo watoto kuliko kuwavunja moyo. Tuwape fursa ya kujaribu chochote kizuri wanachotamani kujaribu, hofu yetu ya kuharibu au kukosea isitufanye tuwanyime nafasi watoto wetu kujaribu, na hata pale wanapokosea tusione kama wamefanya kitu kisichofanywa kabisa, je ninani asiyekosea? Mruhusu kujaribu tena na tena ili aweze kugundua kosa na kujirekebisha. Mpe mtoto wako fursa ya kuibua hoja yoyote anayoiwaza, nyakati nyingine mruhusu akupe ushauri sehemu fulani iliuone anawaza nini. Epuka kuwa mpinzani na mpingaji wa kila anachokifanya au kukisema mtoto wako. Ni jukumu letu kujenga kizazi chenye UJASIRI na KUJIAMINI


Na: Chris Mauki
University of Pretoria
South Africa

3 comments: