Friday, April 20, 2012

JINSI YA KUISHUGHULIKIA HOFU

from samsasali.blogspot.com

Jitambue Ya Chris Mauki...FAHAMU JINSI YA KUISHUHULIKIA NA KUIPUNGUZA HOFU--Part 1


Hofu na mashaka ndio adui namba moja anayefilisi nguvu au nishati ya mwili wa mwanadamu kwa haraka kuliko kitu kingine chochote kile.  Wengi wameathiriwa katika maisha yao ya kielimu, kiafya, kijamii, kikazi na hata kiuchumi kwasababu ya  hofu au mashaka.

Wengi wameshindwa kufikia malengo na ndoto zao katika Maisha kwasababu ya hofu na mashaka.

Mara tu hofu na mashaka yanapoota ndani ya mtu hudumu kwa muda mrefu huku yakileta uharibifu mkubwa katika nafasi, akili, na maendeleo ya mtu huyo kwa ujumla.  Makala au mada  hii itakuwezesha kufahamu kwa kiasi kikubwa mambo unayoweza kufanya ili kuondokana au kupunguza athari za hofu na mashaka na pia kuweza kutoa msaada kwa yeyote anayepitia tatizo hili kwa wakati fulani.

Hofu ni mjumuiko wa kujali kusiko na  sababu yoyote (unnecessary concern) au kusiko na maana yoyote juu ya nafsi au utu wa mtu.  Tunasema  hakuna sababu wala umuhimu wowote kwa sababu kujali huku kumejengwa katika misingi ifuatavyo
-         Mtu kujali sana au kuweka  mawazo sana katika vitu ambavyo viko nje ya uwezo wake.
-         Mtu kuanza  kusikitikia mambo yajayo badala ya kujipanga na kujiandaa kuyakabili pale  yatakapo wadia.
-         Kuweka msisitizo zaidi katika jambo moja na kuyasahau mengine. Anayehofu hudhani kwamba ikiwa kile anachokiwekea msisitizo kitashindikana, basi kila kitu kitakuwa kimeharibika.
-         Mtu kushindwa kutumainia imani aliyonayo  juu ya ufanisi wa jambo fulani.  Hofu yake katika jambo fulani huizidi imani aliyonayo na kwahivyo  hali ya kushindwa kuonekana  dhahiri zaidi kuliko hali ya kushinda.

Kwasababu hofu hujengwa katika fikra  zisizo na maana wala uhalisi wowote, basi njia ya kuiweza hofu hiyo ni lazima  iwe kwa kutumia fikra zenye maana na uhalisi ili kuushinda uwezo wako wa kufikiri kushindwa.
Yafuatayo yatakusaidia kukuwezesha kupunguza kiwango cha hofu katika Maisha.

1.           Jiulize swali “Je nini kinachoniangamiza?”
Hofu ni kitu kinacho angamiza, tena huangamiza kwa viwango na hatua tofauti.  Ngoja nijaribu kukupa mfano wa maelezo.
Hofu kwa lugha ya kingereza ni “worry” neno “worry” limetokana na lugha ya Kidachi lenye  maana ya “Worgen”.  Maana ya neno “worgen” ukiipeleka moja kwa moja katika lugha ya kingereza humaanisha “strangle”. Maana ya neno “strangle” kwa lugha ya kiswahili ni “Kunyonga kwa kamba”. Sasa yamkini hapa unanielewa kwanini ninasema hofu huua au kuangamiza.

Uzuri ni kwamba, hofu haiangamizi pasipo kutoa tahadhari kabla,  baadhi ya tahadhari zinazotolewa katika mchakato wa kuangamizwa  na hofu ni pamoja na hamaki za mara kwa mara, mvi za mapema, baadhi ua upele fulani wa ngozi, vidonda vya tumbo (ulcers), matatizo ya kukosa usingizi, kuhitaji kwenda haja ndogo mara kwa mara n.k.

Swali hili la “ni nini kinachoniangamiza?” litakuwezesha kujitathmini wewe mwenyewe. Katika kulijibu swali hili utaweza kutathmini kwa kujiuliza kuwa “Ni nini katika maisha yangu ambacho nimekipa kipaumbele zaidi kuliko afya yangu na Maisha yangu?  Maana ya swali hili ni ukweli  kwamba kama unahofu katika jambo fulani maana yake hilo jambo au hicho kitu umekipa umuhimu au uzito usiostahili kuliko maisha yako.  Je ni jambo gani au  kitu gani umekipa umuhimu au uzito usiostahili katika maisha yako.  Je ni kazi yako?,  Je ni elimu yako? Je ni ujenzi wa nyumba?  Je ni kibali kwa watu? Je ni watoto wako au mwenza wako?  Je ni malipo ya mkopo uliouchukua? Kumbuka haitakufaidia wala kukuongezea chochote kwa kujiua ukikiwaza hicho kitu, mwisho wasiku mwenye  hasara ni wewe.

Hata mwisho  kama hautapoteza maisha yako lakini ukadhoofisha afya yako, faida yake nini nini?  Na afya yako ikipotea, nini tena utakifanya kuyanufaisha maisha yako?

Kama hofu yako ni kwenye kupata kibali machoni pa watu wanaokuzunguka, labda ofisini, chuoni, mtaani nk.  Kumbuka kuwa watu hao wala hawatajali au kukukumbuka pale utakapokuwa unaugulia wodini au nyumbani kwako kisa ni magonjwa yanayohusiana na hofu.
Labda mfano huu waweza kukusaidia zaidi kuelewa ninacho maanisha.
 Mtu mmoja kijana alimuuliza swali mwanafalsafa (philosopher) mmoja akisema, “Nini kinachokushangaza sana kwa huyu kiumbe binadamu?”

Mwanafalsafa alijibu “Ninamshangaa sana kiumbe mwanadamu kwa sababu hupoteza afya yake kwa kiasi kikubwa sana  akitafuta pesa, na baadae hutumia pesa yake yote akiitibu au kujaribu kuirejesha afya yake iliyo potea katika hofu za Maisha.  Kwa kuihofia kesho yake, mwanadamu huyu ametumia muda wote wa sasa akijiandaa na hiyo kesho, na matokeo yake, kwa kuichosha sana afya yake ameshindwa kuifurahia leo yake na hata hiyo kesho yenyewe huiona kwa taabu sana” (Mwenye ufahamu na afahamu).

 
1.     Acha kuyapa mawazo yako au mitazamo yako umuhimu usiostahili
Hofu, woga na hamaki za mara kwa mara ni alama kwamba unayapa mawazo, fikira na mitazamo yako umuhimu usiostahili.  Maana yake ni kwamba kila unaloliwaza au kulifikiri unalichukulia kua ni halisi, ingawa maranyingine ukweli ni kwamba unavyowaza sivyo.

Hakuna ukweli wala  uthibitisho kuwa kila unacho kiwazakitatokea.
Hizi twaweza kuziita fikra laini, pale ambapo unadhani kuwa kila unachowaza kitatolea.  Mtu mwenye ukichaa, akiwaza kuwa kuna mtu anataka kumpiga risasi atakimbia huku na huko kujificha. Wakati ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho. Wewe sio kichaa, kwanini uweke vyote unavyoviwaza  kama vile ni dhahiri? tena hususani vile vitu vibaya?

Tabia sugu nyingi walizonazo watu husababishwa na fikra, vile wanavyowaza.  Usiruhusu mawazo yako yakufanye mtumwa.  Mawazo ya kitaalam yanaonyesha kwamba kama ukiweka  mawazo yako sana katika kitu fulani, inaweza kuishawishi tabia au utendaji wako katika hali  ambayo yaweza kuanza kufanya hofu zako kuanza kuwa kweli. Ni kwasababu hii ndiyo maana, unashauriwa kuweka  mawazo na fikra zako zote kwenye vitu ambvyo ni vya maana.

2.     Usijiogopeshe kwa vitu ambavyo hutokea kwa nadra sana
Njia bora ya kuyatengeneza mawazo yetu yanayofikiri sana juu ya hatari ambazo kutokea kwa nadra sana ni kwa kuwaza kuwa wewe hautakuwepo pale hatari hiyo itakapo tokea katika eneo hilo, na hivyo haitakuathiri.

Kwanini uwaze kwamba wewe  una bahati mbaya  sana na vyote vibaya vitakapotokea vitakukuta wewe tu.  Najua inawezekama  kabisa lakini nafasi za kuwezekana huko ni ndogo sana.  Mfano. Kwanini uwaze kuwa unapotembea msituni peke yako, mti unaweza kukuangukia.  Au unapokukwa kwenye ndege au meli, ajali yaweza kutokea, au hata unapokuwa safarini kwa gari, jiulize mabasi mangapi yametoka kule unakotokea na kufika salama kule unakokwenda bila shida yeyote, wewe je huwezi kuwa mmoja wa waliokuwa salama?

Kuna mambo mengi ya kuogopesha yanayotokea katika maisha yetu ya kila siku, na kama ukiogopa na kuhofu kila kitu na kutofuata ushauri unaotolewa hapa, basi kila siku utatembea na kuishi kwa hofu tu.

No comments:

Post a Comment