MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Kwanza
Jambo la kwanza
Kuoa au
kuolewa kunabadilisha uhusiano
wako na wazazi wako.
Mwanzo.2:24 anasema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake
na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili moja”.
Ukiangalia (Zaburi.45:10-11) anasema, “Sikia binti
utazame (maana yake anazungumza na msichana) utege sikio
lako. Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako na mfalme
atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako naye umsujudie”.
Najua watu
wengi sana wanataka waingie kwenye ndoa, waoe au waolewe, lakini
uhusiano wao na wazazi wao usibadilike, haiwezekani. Biblia
imeweka wazi kabisa, unataka kuoa, mwanamume lazima kwanza
aachane na baba yake na mama yake, maana yake kuna mabadiliko.
Kuna mabadiliko mahali pakuishi, kuna mabadiliko juu ya mtazamo
wako wa kwanza wa maisha yako. Mke wako hawezi kuwa mama yako,
na mume wako hawezi kuwa baba yako. Mke wako anakuwa mke wako
na si mama yako. Mume wako anakuwa mume wako na si baba yako.
Na kabla
hujafikia maamuzi ya namna hiyo - ukiingia kwenye ndoa, ndoa
yako itakuwa ngumu. Maana inawezekana unaishi vizuri na wazazi
wako, kiasi ambacho maamuzi yako yoyote unayofanya lazima
ushirikiane nao, na hiyo ni hatua nzuri kabisa. Lakini
ukiishaingia kwenye ndoa, mtu wa kwanza wakushirikiana naye ni
mke wako kama umeoa, na ni mume wako kama umeolewa lakini, sio
baba yako, sio mama yako.
Na wazazi
wengine wasingetaka kuona kwamba unakuwa mbali nao kwa jinsi hii,
wanataka waendeleze maamuzi yao na utawala wao waliokuwa nao juu
yako mpaka kwenye ndoa yako, haiwezekani. Biblia inakataa. Sasa
ukisoma ile Mwanzo unaweza ukafikiri ni wanaume tu wakioa ndio
wanatakiwa watoke, waachane na wazazi wao, lakini Zaburi
45:10,11 inatuambia wazi kabisa, inasema, “Sikia, binti,
utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba
yako. Naye Mfalme atautamani uzuri wako, Maana ndiye bwana wako,
nawe umsujudie”.
Sasa
haimaanishi usiwasalimie, haimanishi usiwasaidie, lakini
ningekuwa nazungumza kwa kiingereza ningekuambia, “your
priorities must change” lazima ubadilike jinsi ambavyo
unaweka kipaumbele katika watu ulio nao.
Unapoamua
kuolewa, wa kwanza sio baba yako wala sio mama yako, wa kwanza
ni mume wako baada ya Yesu. Katika mahusiano ya kibinadamu
anayekuja pale wa kwanza baada ya Yesu moyoni mwako ni mume wako.
Ikiwa hujafikia maamuzi ya namna hii moyoni mwako basi bado
hujafikia utayari wa kuolewa. Na ina madhara yake magumu. Maana
biblia inasema, kabla hujawasahau watu wako na watu wa nyumba ya
baba yako, mume wako hawezi kuutamani uzuri wako, ukitaka
autamani uzuri wako lazima uwasahau kwanza watu wa nyumbani kwa
wazazi wako.
Sasa kuna
tofauti ya kupenda na kutamani. Kabla hujaolewa au kabla hujaoa
huruhusiwi kutamani. Lakini ukiisha oa unaruhusiwa kutamani
lakini mke wako tu. Ukiishaoa kutamani mke wako ruksa, na biblia
imeweka vizuri kabisa, na ukiishaolewa kutamani mume wako ni
ruksa. Lakini biblia imeweka utaratibu wa ajabu sana kwamba, ili
mume amtamani mke wake, lazima mke wake awasahau kwanza watu wa
nyumbani mwa wazazi wake. Hiki ni kigezo kigumu sana.
Ndio maana
unaweza ukakuta mtu ana mke mzuri sana lakini hamtamani.
Unaweza ukafikiri labda ni kwa kuwa hajajipamba vizuri; lakini
hata kama atajipamba, atajikwatua kuanzia asubuhi mpaka jioni,
- anaweza hata akatumia muda mwingi kwenye kioo kuliko kwenye
maombi akijitengeneza, lakini bado mume wake asimtamani; kwa
nini? Kwa sababu ndani yake hajaachia watu wa nyumba ya wazazi
wake. Au watu wa nyumba ya baba yake wana nafasi kubwa moyoni
kuliko mume wake.
Ni
mabadiliko ambayo lazima uyatarajie, watu wengi sana huwa
hawafikirii hayo, wanafikiri ni kitu rahisi. Unaweza sasa
ukaelewa kwa nini watu wengine ikifika siku ile ya “send off”,
yaani ya kum’send’ msichana ‘off’ asikae tena nyumbani kwa baba
yake, hiyo siku ni ngumu sana kwa wazazi. Kwa sababu wanajua,
wanaagana na msichana wao, mahusiano yao waliokuwa nayo toka
mwanzoni, tangu alipozaliwa, alipokuwa tumboni mpaka wakati huo
yanabadilishwa, yanajengwa mengine, sasa anakwenda kuwa mke wa
mtu, hawawezi tena kuingilia maamuzi juu yake, amefunga agano
mahali pengine.
Unakuta
siku hiyo wazazi wengine wanalia, unakuta vijana wengine wanalia,
wasichana wengine wanalia. Usije ukafikiri ni kitu rahisi. Ndani
ya nafsi kuna vitu vinaachana, kati ya wazazi na wale watoto
wanaoana.
|
No comments:
Post a Comment