MAMBO YA
KUTAFAKARI KABLA YA KUFANYA
UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Wiki ya
Pili
Jambo la Pili
Unapoamua
kuoa au kuolewa, fahamu ya kwamba hiyo ndoa
inakuunganisha na kukuingizakatika familia nyingine.
Unafahamu
watu wengi sana wakioa au kuolewa wanafikiria tu mahusiano ya
wao wenyewe tu; na hii ni hatari sana. Kwa sababu unapooa
unaingia kwenye undugu na familia nyingine kabisa tofauti, na
sio mahusiano ya kwenu tu wawili. Ninyi ni kigezo tu cha
kuunganisha hizo familia mbili, lakini mkiishaoana hizo familia
zenu mbili ni ndugu kuanzia wakati huo.
Ndio
maana unapofika unataka kuoa au kuolewa, sio suala la kumtazama
kijana tu, au kumtazama msichana yeye mwenyewe tu; kwa mfano
alivyosoma, lakini ni lazima pia utazame na hali ya familia yake
ili ujue unajiingiza kwenye familia ya namna gani. Unapofika
kwenye masuala ya namna hiyo kuna vitu vingi sana vya kuangalia.
Unaweza
ukaingia kwenye familia ambayo ni wavivu, mimi ninakuambia jasho
litakutoka ukioa msichana wa namna hiyo; au ukipata kijana toka
kwenye familia ya namna hiyo. Itakuwa kazi sana kumshawishi
mwenzako juu ya kujishughulisha na maisha. Maana inategemea; kwa
kuwa unaweza kuoa msichana hata kusonga ugali hajui. Sisi kwenye
nyumba ya baba yetu, hatuna msichana, tumezaliwa watoto wa kiume
watupu, msichana wa kwanza kuingia kwenye familia yetu ni mke
wangu.
Lakini
mama yetu alikuwa na bidii ya kutufundisha kila kitu,
alitufundisha kupika, alitufundisha kufuma, alitufundisha kusuka
nywele. Kwa hiyo nilijifunza kwanza kusuka tatu kichwa. Lakini
sikuanzia kujifunzia kusuka nywele kwenye kichwa cha mtu, bali
nilijifunzia kwenye majani; wao wakikaa wanasuka hapo na sisi
tuko hapo tunafundishwa jinsi ya kusuka kwenye majani.
Sasa
wengine hawapati nafasi ya namna hiyo, na ni mbaya zaidi kwa
wasichana. Mungu amenipa nafasi ya kuwa na watoto wakike watatu
na wa kiume mmoja, itakuwa ni aibu kwetu kama wazazi, ikafika
wakati wanaingia katika ndoa zao na hawajui kupika ni aibu; kwa
hiyo lazima wajue kupika. Maana kwa kujua hilo anaonyesha
anatoka familia ya namna gani, na imemlea kwa namna gani!
Unaweza
ukafikiri unamlea mtoto wako vizuri, maana siku hizi kuna shida
ya kuwa na wafanya kazi majumbani mwetu. Ukishakuwa na
mfanyakazi nyumbani basi watoto wengine hawafanyi kitu, wakati
mwingine wanakula chakula na wanaacha sahani hapo hapo mezani.
Kuna
watoto wengine inakuwa mpaka yuko sekondari hawezi kufua nguo
zake. Kwa kuwa nyumbani kama hakuna wa kumfulia basi kuna
mashine za kufulia. Huko unakokwenda kuolewa inawezekana hata
mashine ya kufulia hawajawahi kuiona! Unafika pale na unauliza
mashine iko wapi, wanakuambia yakufanyia nini, - ya kusagia
mahindi? Maana ndio wanayoijua kuwa ndio mashine!
Hujui
hata namna ya kushika kioo cha taa ya chemli wala namna ya
kuiosha kule ndani lile vumbi likaondoka. Inawezekana mwingine
umezaliwa kwenye nyumba yenye umeme, lakini utakapokuwa katika
ndoa unaenda kwenye nyumba ambayo haina hata umeme, unafika kule
na unashangaa kweli maana hujui hata namna kuwasha taa ya chemli!
Kwa hiyo tunawaambia watoto wetu suala la kujifunza hivi vitu
sio suala la kuchagua, hata kama kuna mtu pale nyumbani wa
kuwasaidia, ni lazima wajue kufanya kazi!
Nilienda
kwenye mkoa mmoja wakasema, sisi ukitaka kuoa kwenye nyumba ya
mtu, ukitaka kujua huyo msichana amelelewa vizuri au vibaya
wakasema usimtazame alivyovaa. Badala yake wanafika kwenye
uwanja wa nyumba ya wazazi wake, na wanaangalia ile barabara
inayokwenda nyumbani kwao, na wakiikuta chafu, basi wanajua
huyu msichana ni mchafu, hawahangaiki tena kuja kuzungumza,
wanajua hapa kama tunaamua kuoa tujue tunacho oa, huyu msichana
ni mchafu!
Ukienda
kuoa kwenye familia nyingine utakuta wanasumbuliwa na ugonjwa wa
kurithi, na usipojua kitu cha kufanya unaweza ukapata shida sana.
Lakini ninachotaka kukuambia ni kwamba, uamuzi wa kuoa au
kuolewa unakuingiza kwenye familia nyingine kabisa, na
inaunganisha hiyo familia yao na familia yako; kwa hiyo hayo
sio maamuzi madogo. Kumbuka unapooa au kuolewa unawaingiza watu
katika famila ambazo kama usipokuwa mwangalifu inaweza ikaleta
shida sana, lakini pia inaweza ikaleta baraka!.
|
No comments:
Post a Comment